Kitulo FM

Wananchi washiriki zoezi la kusafisha uwanja Kituo cha Afya Lupalilo

January 25, 2023, 12:33 pm

Wananchi wa Kijiji cha Lupalilo kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya na Kamati ya Siasa Wilaya wameshiriki zoezi la kufanya usafi na kuandaa mazingira rafiki eneo la Kituo cha Afya Lupalilo kilichopo Kijiji cha Lupalilo Wilaya ya Makete.

Costantino Swalo na Amie Sanga wakieleza kuhusu ujenzi wa Kituo hicho wamesema Serikali imeona mbali kutibu jeraha la kupunguza gharama za huduma na kusafiri kwenda kutibiwa umbali mrefu kwa gharama kubwa katika Hospitali binafsi.

Ibrahim Sanga Mwenyekiti wa Kamati ya manunuzi Kituo cha Afya Lupalilo amempongeza Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya.

Diwani Kata ya Lupalilo Mhe. Imani Mahenge ameishukuru Serikali kwa kujenga kituo hicho na kutambua umuhimu wa huduma ya Afya kwa wananchi wake.

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Makete William Makufwe akizungumza mbele ya Kamati ya Siasa ya Wilaya (CCM) amesema Serikali imetoa Milioni 500 kujenga kituo hicho na tayari imeshaleta wataalamu 7 kwa ajili ya kutoa huduma kwenye Kituo hicho.

Kwa upande wa wajumbe wa Kamati hiyo ya Siasa wamezipongeza Kamati zote zinazoshiriki katika usimamizi wa ujenzi wa Kituo hicho huku wakiishukuru Serikali na Mbunge Jimbo la Makete Mhe. Festo Sanga kwa ujenzi wa kituo hicho.