Kitulo FM

Mwenyekiti CCM Wilaya ya Makete aipongeza Wizara ya Maji

January 24, 2023, 7:11 am

Kamati ya Siasa Wilaya ya Makete ikiongozwa na Clement Ngajilo imeipongeza Wizara ya Maji ikiongozwa na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso, Katibu Mkuu Mhandisi Anthon Sanga kwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa Maji (Kinyika-Matamba).

Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Bilioni 2 ambapo mpaka sasa umejengwa kwa Bilioni 1 umeanza kutoa huduma kwa wananchi wa Kata 3 ambazo ni Kinyika, Matamba na Mlondwe na kufanikiwa kutatua changamoto ya Maji kwa wananchi zaidi ya elfu 15.

Akieleza kuhusu mradi huo Martin Luvanda kutoka Ofisi ya RUWASA Makete amesema Serikali ilitoa fedha hizo kwa lengo la kuwanusuru wananchi wa kata hizo kuepukana na adha ya Maji na sasa hakuna shida ya Maji katika Bonde hilo la Matamba.

Pia ameeleza kuwa Serikali inatarajia kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa Mfumo wa Maji kwa wananchi na kufunga dira za maji ili kuhakikisha hakuna maji yanayopotea kiholela.