Kitulo FM

Wananchi 50 Tandala wakabidhiwa Hati Miliki za Ardhi

January 20, 2023, 7:00 pm

Ofisi ya Ardhi mkoa wa Njombe imeendesha zoezi la kukabidhi hati zipatazo Hamsini kwa wananchi wa kijiji cha Tandala wilayani Makete pamoja na kusikiliza changamoto za wananchi juu ya zoezi hilo leo Disemba 20 mwaka huu.

Emmanuel Mkiwa kutoka ofisi hiyo amesema zoezi la kugawa hati 50 zilizokuwa zimeandaliwa kwa wale waliolipia limefanyika vizuri hivyo amewataka wananchi kuzingatia elimu wanayopewa juu ya umuhimu wa kumiliki ardhi kisheria kwa kuwa na hati.

Yusuphu Ilomo ni mwenyekiti wa kijiji cha Tandala amesema zoezi hilo limefanikisha kumaliza mgogoro uliokuwepo kwa baadhi ya wananchi wa kitongoji cha Posta.

Mwalimu Beni Mbilinyi na Lususu Mbilinyi ni baadhi ya wananachi wa Tandala waliojitokeza kuchukua hati zao ambapo wamezungumzia umuhimu wa kuwa hati huku wakiomba serikali kuongeza kasi ya kuyafikia maeneo mbali mbali wilayani Makete ili wananchi waweze kuongeza thamani ya maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuombea mikopo benki ili waongeze kipato cha mwananchi mmoja mmoja.