Kitulo FM

Wazazi wanashawishi Wanafunzi wafeli Mitihani

January 17, 2023, 9:58 am

 

Wananchi wa Usagatikwa wakiwa kwenye mkutano

Wazazi kijiji cha Usagatikwa Kata ya Tandala na Ibaga Kata ya Mang’oto wamebainika kushawishi wanafunzi wafeli mitihani ya Darasa la Saba kwa maksudi.

Kaimu Afisa Elimu Idara ya Msingi Wilaya ya Makete Mwalimu Bakari Msuya amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wazazi kushawishi watoto wanaohitimu darasa la saba wafeli mitihani kwa maksudi.

Msuya ameeleza kuwa wazazi hao walibainika na kuchukuliwa hatua huku wakiagizwa kuhakikisha watoto hao wanapelekwa vyuo mbalimbali vya ufundi ili waweze kujiendeleza kielimu.

Afisa Tarafa ya Lupalilo ambaye anasimamia Kata ya Tandala, Mang’oto, Lupalilo, Iwawa na Isapulano Augustino Ngailo amesema walibaini changamoto hiyo baada ya wanafunzi 33 waliomaliza darasa la saba shule ya Msingi Usagatikwa 19 kati yao kufeli mtihani

Pia mwanafunzi mmoja aliyekuwa akishika nafasi ya pili mitihani ya majaribio ya Kata Mang’oto (akitoka shule ya Msingi Ibaga) kufeli masomo ya kuhitimu darasa la saba jambo lililowafanya wawakamate wazazi wake na kuwauliza ndipo walipoeleza kuwa walimshawishi mwanafunzi afanye vibaya mitihani yake ya mwisho.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Makete William Makufwe amekuwa akikemea mara kwa mara suala la wazazi kushawishi wanafunzi kufeli kila anapokuwa akifanya mikutano ya hadhara na wananchi katika vijiji mbalimbali wilayani hapa na kuahidi hatua zaidi zitakuwa zikichukuliwa kwa mzazi/mlezi yeyote atakayebainika kushawishi mwanafunzi kufeli mitihani.