Kitulo FM

Idadi ya wanafunzi kuripoti shule bado changamoto

January 17, 2023, 8:57 am

 

Wananchi wa Kijiji cha Usagatikwa wakiwa katika picha siku kadhaa zilizopita kwenye mkutano wa kijiji

Kijiji cha Usagatikwa wilayani Makete mkoani Njombe kipo kwenye hatari ya kukosa wasomi katika siku zijazo kutokana na wanafunzi wanaopangiwa kuanza kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Lupalilo wengi wao kutohitimu kidato cha Nne

Akitoa taarifa ya ripoti ya wanafunzi wa kidato cha kwanza 2023 katika Kikao cha kamati ya Maendeleo ya Kata ya Tandala kwa robo ya piliĀ  Januari 16, 2023 Kaimu Mkuu wa shule ya sekondari Lupalilo Mwl. Lunanilo Kilatu amesema hali haikuwa nzuri Ijumaa ya wiki iliyopita kwani walikuwa wameripoti kwa asilimia 44 hali iliyopelekea taarifa kutumwa kwa mtendaji wa kata lakini hadi kufikia januari 16.2023 kumekuwa na ongezeko la wanafunzi walioripoti kwa asilimia 73 kwani kiujumla wamesharipoti wanafunzi 91 kati ya 124 waliopangwa kwenye shule hiyo

Mwalimu huyo amesema kumekuwa na changamoto ya wanafunzi hao baada ya kuripoti shuleni kusema kuwa hawataki kusoma jambo ambalo ameomba ushirikiano kwa serikali na wazazi kuwadhibiti watoto wao ili wasome kwao wao kama shule wamewakatalia na kuwaambia kuwa hakuna mtoto atakayeacha shule

Kaimu Mkuu huyo wa shule hakusita kuzungumzia suala la wanafunzi wanaopangiwa shuleni hapo kutoka kijiji cha Usagatikwa kutoripoti shuleni na hatari ya kijiji hicho kukosa wasomi

Hali hiyo ya kijiji cha Usagatikwa imeungwa mkono na Afisa Elimu Kata ya Tandala Mwl. Eskaka Sanga ambapo amelazimika kutoa takwimu za matokeo ya kuhitimu elimu ya msingi 2022 kwa shule za kata yake ambapo kwa Tandala walifanya mtihani watoto 40 wakafaulu 37, Ihela walifanya mtihani wanafunzi 25 wakafaulu 23, Ikonda walifanya mtihani 56 waliofaulu ni 53 na kwa Usagatikwa walifanya mtihani wanafunzi 33 na wakafaulu 14 sawa na asilimua 42 ambapo ukilinganisha na mwaka juzi Usagatikwa walifanya mtihani watoto 26 na wakafaulu 13 sawa na asilimia 71

Afisa Elimu huyo amesema katika utafiti walioufanya katika kijiji hicho pamoja na sababu zingine za walimu lakini wamebaini kuwa tatizo lipo kwa wazazi kwani wanafunzi hao wamekuwa wakifanya vizuri mitihani yao mingine lakini wanashawishiwa na wazazi wafanye vibaya kwa kuwa baadhi ya wazazi hawapendi watoto wao wasome na pia wale wanaofaulu hawamalizi kidato cha nne wote.