Kitulo FM

Msikae Ofisini Fuatilieni Ufundishaji na Ujifunzaji Mashuleni: Dkt. Dugange

January 9, 2023, 6:02 pm

 

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo J. Dugange akiwa katika Mkutano wa tathmini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa Elimu msingi na sekondari Njombe

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo J. Dugange amewataka viongozi wa Elimu ngazi ya Shule, Kata, Halmashauri na Mikoa kutokaa ofisini bali wafuatilie ufundishaji na ujifunzaji shuleni kwa kushauriana na walimu na kuhakikisha wanafunzi wanapata umahiri uliokusudiwa katika masomo yote.

Dkt. Dugange ametoa maelekezo hayo Leo tarehe 9 Januari 2023 mkoani Njombe katika Mkutano wa tathmini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa Elimu msingi na sekondari uliowakutanisha viongozi wa Elimu ngazi zote.

“Viongozi wa Elimu jielekezeni zaidi kufuatilia ufundishaji wa walimu darasani na kutatua kero za walimu kwenye maeneo yao ya kazi na mhakikishe mnaimarisha uwajibikaji wa watumishi wote katika ngazi zote ili kuongeza tija katika utendaji wa kazi” amesisitiza Dkt. Dugange

Viongozi mbalimbali wa Elimu wakimsikiliza Naibu Waziri Mhe. Dugange

Amewataka Walimu kujiwekea malengo yao binafsi katika masomo wanayofundisha na kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeshindwa kupata umahiri uliokusudiwa katika somo lake analofundisha.