Kitulo FM

Mzazi atakayemtorosha mwanafunzi atasoma yeye-Dc Sweda

December 30, 2022, 8:22 am

 

Mkuu wa Wilaya ya Makete (Kulia) akionyesha samani zilizopo kwenye vyumba vya madarasa Iwawa Sekondari

Mkuu wa Wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda amewataka wazazi kuacha tabia ya kutowapeleka wanafunzi shule na kuwatorosha kwenda mijini kufanya biashara huku wakijua wanawanyima watoto haki ya Msingi ya kupata elimu.

Mhe. Sweda amesema mzazi/mlezi ambaye hatompeleka mwanafunzi kidato cha kwanza bila sababu za Msingi atachukuliwa hatua za kisheria haraka iwezekanavyo au atalazimika kusoma yeye mwenyewe kama mzazi kwa niaba ya mtoto.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema tayari madarasa yamekamilika kwa 100% kwa ajili ya kupokea wanafunzi watakaoripoti kidato cha kwanza mwaka 2023 na miundombinu muhimu yote imekamilika.

Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Iwawa Staphord Mwandelile amesema shule hiyo kupitia pochi la Mama Samia suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipokea fedha Mil. 40 kujenga vyumba viwili vya madarasa lakini wamefanikiwa kuongeza na chumba kimoja kwa ajili ya ofisi ya walimu kwa fedha hiyohiyo.

Mwandelile amesema kujengwa kwa madarasa hayo kumefuta kabisa adha ya upungufu wa madarasa shuleni hapo na sasa wapo tayari kupokea wanafunzi wapya kidato cha kwanza 2023.

Lucy Sanga mkazi wa Kijiji cha Mago Kata ya Lupalilo kwa niaba ya wazazi/walezi amesema wapo tayari kupeleka watoto kidato cha kwanza na kuwasihi wazazi kufanya maadalizi mapema ili kuhakikisha ifikapo tarehe 9 Januari 2023 wanafunzi wote wanaanza masomo.

Jumla ya wanafunzi 2,408 kati yao wasichana 1,224 na wavulana 1,184 wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule mbalimbali Wilayani Makete Mkoani Njombe.