Kitulo FM

Afariki Dunia kwa kusombwa na Maji Makete

December 30, 2022, 6:39 am

 

Picha ni wananchi wa Kijiji cha Lupalilo wakiwa nyumbani kwa marehemu kabla ya mazishi kufanyika.

Bibi anayekadiriwa kuwa na miaka zaidi ya 80 afariki kwa kusombwa na Maji kijiji cha Lupalilo Wilaya ya Makete akijaribu kuvuka mto juu ya daraja dogo katika mto Idetele unaotenganisha Kijiji cha Lupalilo na Ilevelo.

Baadhi ya wanandugu wamesema tukio hilo limetokea tarehe 28 Disemba majira ya mchana kati ya saa 8-9 alasiri kwani muda wa saa 7 mchana walikuwa naye Bibi huyo mtaani kabla hajarudi nyumbani kwake.

Safina Sanga Mwenyekiti wa Kijiji cha Lupalilo amesema tukio hilo limetokea kwenye Kitongoji cha Mtakuja baada ya mvua kubwa kunyesha na huenda Marehemu alikuwa anataka kuvuka mto ndipo alipozidiwa na kusombwa na maji yaliyojaa mto Idetele na kuvutwa umbali wa zaidi ya Kilomita 1.

Mwenyekiti huyo ameendelea kuwasihi wananchi kuwa watulivu na kuchukua tahadhari wakati ambapo mvua nyingi zinanyesha katika Wilaya ya Makete.

Jeshi la Polisi Makete limefika kwenye Kitongoji hicho kwa ajili ya uchunguzi zaidi huku taratibu za mazishi zikielekezwa kuendelea ambapo Jeshi hilo limewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari wakati wote ambapo mvua kubwa zimekuwa zikinyesha mfululizo kutwa nzima na hata usiku.