Kitulo FM

IJUE SHERIA

October 26, 2021, 6:22 pm

Kwenye Kipindi cha Ijue Sheria kinachorushwa kila siku ya Jumatatu saa 2:00 Usiku mpaka saa 3:00 Usiku Mkurugenzi Mtendaji Shirika la wasaidizi wa Kisheria Wilaya ya Makete (MAPAO) Mch. Denis Sinene ametupiga msasa kuhusu majukumu.

(i) Kuwakilisha wananchi katika Halmashauri, Diwani huwakilisha wakazi wote wa Kata yake hivyo anatakiwa kuwa karibu na wapiga kura wake na kufikisha mbele ya Halmashauri na Kamati zake vipaumbele vya wananchi ili vijadiliwe na kutolewa maamuzi.

(ii) Kuhamasisha wananchi katika kulipa kodi na ushuru wa Halmashauri.

(iii) Kusimamia matumizi ya Fedha za Halmashauri, Diwani anatakiwa kuhakikisha Fedha za Halmashauri zinatumiwa kwa madhumuni yaliyokusudiwa na sio vinginevyo.

(iv) Kuwa kiungo kati ya Halmashauri na ngazi za msingi za Serikali za Mitaa. Diwani ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata. Atumie mamlaka hayo kuwasilisha kwenye Halmashauri maamuzi ya Kata yake na vile vile kuwasilisha kwenye Kata maamuzi ya Halmashauri.

(v) Kuhamasisha wananchi kuhusu vita dhidi ya umaskini. Katika kulitekeleza hili ni lazima ajue kwa ufasaha hali ya kiuchumi na kijamii inayowakabili wananchi wake na kushirikiana nao ili kupanga mipango endelevu ya kujikwamua.

(vi) Kufuatilia utekelezaji wa mipango yote ya wananchi na ya Halmashauri. Ili kutimiza jukumu hili ipasavyo, Diwani anatakiwa kufuatilia utekelezaji wa miradi yote ndani ya Kata yake ambalo ni jimbo lake la uchaguzi bila kudai malipo yoyote toka kwenye Halmashauri au wadau wengine. Kimsingi hii ndiyo kazi ambayo Diwani aliahidi kuitekeleza wakati wa kampeni.

(vii) Kutetea Maamuzi ya Halmashauri. Wakati wa majadiliano ndani ya Halmashauri, Diwani ataelekeza na kutetea maoni yake au ya wakazi wa eneo lake.

Hata hivyo, iwapo uamuzi utakaofikiwa na wengi utakuwa kinyume na matarajio yake atalazimika kuunga mkono maamuzi ya wengi yaliyofikiwa kidemokrasia.

(viii) Kuzingatia misingi yote ya Utawala Bora wakati wa kutekeleza majukumu yote ya Udiwani.

Mchungaji Denis Sinene Mkurugenzi wa Wasaidizi wa Kisheria Makete.