Karagwe FM

Zaidi ya watoto elfu 99 kupata chanjo ya polio Karagwe

11 September 2023, 12:11 pm

Mratibu wa chanjo Halmashauri ya wilaya ya Karagwe mkoani Kagera bi Modester Kibona. Picha na Eliud Henry

Watoto 99,159 wilayani Karagwe watakuwa miongoni mwa watoto 3,250,598 wenye umri wa chini ya miaka minane watakaopata chanjo ya kinga ya polio katika kampeni ya chanjo kitaifa Septemba 21-24 mwaka huu.

Na. Tumaini Anatory

Kwa mujibu wa mratibu wa chanjo katika halmashauri ya wilaya ya Karagwe mkoani Kagera bi Modesta Kibona watoto wote wenye umri chini ya miaka 8 wapatao 99,159 watapata chanjo kupitia kampeni maalumu ya siku nne itakayofanyika nyumba kwa nyumba kuanzia Septemba 21-24 mwaka huu.

Akieleza zaidi mambo yanayosababisha maambukizi ya polio, bi Modester ameitaka jamii kuzingatia kanuni za afya kwa kuwa pia ugonjwa huu huambukizwa kwa kula uchafu

Chanjo ya polio inafanyika kitaifa mwezi huu wa Septemba kutokana na maelezo ya Waziri wa afya Ummy aliyoyatoa kwa vyombo vya habari hivi karibuni akifafanua kuwa maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Polio yametolewa taarifa pia katika nchi zinazopakana na Tanzania mfano Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia na kusababisha tishio na hatari ya maambukizi ya Virusi vya ugonjwa wa Polio kwa nchi yetu hususani katika Mikoa inayopakana moja kwa moja na nchi hizo ambayo ni Mikoa sita ya Rukwa, Kagera, Kigoma, Katavi, Songwe na Mbeya