Karagwe FM

Wapewa siku 90 kuwapisha wafugaji

6 November 2021, 11:38 am

Wakulima waliovamia ardhi ya kijiji cha Kashanda kata ya Nyakakahanga wilayani Karagwe  wamepewa miezi mitatu kuvuna mazao yao mahindi na maharage na kisha kuondoka katika kijiji hicho ili kuwaacha wafugaji waendelee na shughuli zao.

Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Kagera ikiongozwa na mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Generali Charles Mbuge awali aliwapa wiki mbili wakulima lakini baada ya wakulima hao kuomba waongezewe muda akawapa muda wa miezi mitatu ili wavune mazao yao na kuondoka.

Kashanda Karagwe

Akiongea katika mkutano maalumu wa usuluhisho wa mgogoro baina ya wakulima na wafugaji kijijini hapo mwenyekiti wa chama cha wafugaji Mchungaji Dk.Godfrey Aligawesa amesema kuwa tangu wakulima walipovamia ardhi imekuwepo migogoro ya kubambikiziwa Kesi ambapo wakulima wamekuwa wakikamata ng’ombe kuwa wamekula mazao na wafugaji wanatozwa fedha na limekuwepo tatizo la kuua mifugo na hadi sasa ng’ombe 110 waliuliwa.

Diwani wa kata ya Nyakakahanga Charles Beichumila amesema kuwa, kata yake ina vijiji vinne vya Nyakakahanga, Omurusimbi, Bisheshe na Kashanda kwamba kijiji hicho ni cha wafugaji.

Ameongeza kuwa wakulima walivamia eneo hilo mwaka 2016 licha ya oparasheni ya kuwaondoa kufanyika bila mafanikio na mwaka 2019 hadi  mwaka 2020 kipindi cha uchaguzi walirudi tena kwa kuuziwa na watu wachache kila ekari Sh laki moja na elfu 20.

Aidha watu watano akiwemo mwenyekiti wa kijiji cha Kashanda wanaotuhumiwa kuuza ardhi wamekamatwa na watafikishwa katika vyombo vya sheria.