Karagwe FM

World Vision Tanzania Kanda ya Kagera yatoa faraja Missenyi

2 May 2021, 12:59 pm

Shirika la World Vision Tanzania Kanda ya Kagera mradi wa Missenyi limekabidhi msaada wa vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 12.5 kwa zaidi ya watu 300 wanaoishi kwenye kambi baada ya kuhama makazi yao

Akikabidhi msaada huo kwa Mwenyekiti wa Kamati ya maafa wilaya ambaye pia ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo bw.Innocent Mukandala, Kaimu Meneja wa World Vision Tanzania Kanda ya Kagera Atugonza Kyaruzi amesema kuwa mradi kwa kushirikiana na wafadhili wametoa unga wa mahindi tani 1.3, maharage kilo 260, Sukari kilo 260, Blanketi 156 na vyandarua 156

Bi Atugonza ametaja vitu vingine walivyotoa kuwa ni ndoo 10 za kuwekea maji ya kunawia mikono dawa za kutibu maji na kwamba pia wametenga kiasi cha shilingi milioni 1.5 zitumike kuelimisha jamii juu ya kujilinda katika kipindi cha mvua nyingi zinazosababisha mafuriko

Baadhi ya wananchi wakipokea msaada wa vyakula na mahitaji mengine

Baada ya kupokea msaada huo wenye thamani ya shilingi milioni 12,528,000, Mwenyekiti wa Kamati ya maafa wilaya ya Missenyi Innocent Mukandala amelishukuru Shirika hilo kwa kutoa mahitaji hayo na akatoa wito kwa wadau wengine kuendelea kujitokeza ili kusaidia wahanga kwa kuwa bado mvua zinaendelea kunyesha

Kaimu Meneja wa World Vision Kagera Bi Atugonza Kyaruzi akikabidhi msaada wa vyakula kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Missenyi bw. Innocent Mukandala

Mkandala pia ametoa wito kwa wakazi wa Kyaka Bunazi kujenga nyumba kwakuzingatia jiografia ya eneo hilo ili kuepuka tatizo la nyumba zao kujaa maji linalojitokeza karibu kila msimu wa mvua zinaponyesha nyingi huku akisema kuwa wanaomkakati wakuchimba mitaro itakayosaidia kuelekeza maji mto Kagera ili kuepusha kadhia hiyo

Baadhi ya Wananchi wanaoishi kwenye kambi iliyoko Kigango cha Omukitwe wameshukuru msaada waliopewa pia wakaomba kupewa misaada mingine zaidi ya kibinadamu huku wengine ambao nyumba zao zimeanguka wakiomba kusaidiwa vifaa vya Ujenzi

Baadhi ya wananchi wakiwa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Missenyi Innocent Mukandala (Aliyevalia koti jeusi)