Karagwe FM

Sekondari 15 kati ya 22 zafanikisha Lishe

19 April 2021, 4:32 pm

Afisa Elimu sekondari wilayani Missenyi mkoani Kagera Mwl Saverina Misinde amezipongeza shule za sekondari 15 za serikali zinazotoa huduma ya chakula cha mchana ili kuwawezesha wanafunzi kujifunza vizuri wakiwa wameshiba

Pongezi hizo amezitoa hivi karibuni wakati Kamati ya fedha Utawala na Mipango ilipotembelea shule ya sekondari Gablanga na shule ya sekondari Kilimilile ili kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa

Baadhi ya wanafunzi wa sekondari wakifurahia mlo wa mchana

Ameongeza kuwa Lishe bora ni muhimu sana kwa mwanafunzi kwakuwa akiwa na njaa atasinzia darasani, hawezi kumsikiliza kwa ufasaha Mwalimu wake hivyo akatoa wito kwa viongozi kuhamasisha wazazi wahakikishe Shule zote za Msingi na Sekondari zitoe chakula kwa wanafunzi

Sauti ya Afisa Elimu Sekondari (W) Missenyi Saverina Misinde

Mwalimu Johachim Mwombeki Mutembei ni Mkuu wa Shule Msaidizi wa Shule ya Sekondari Gablanga amesema kuwa wamefanikiwa kutoa chakula kwa wanafunzi baada ya wazazi kuhamasika wakakubaliana kuchangia mahindi,maharage na fedha shilingi elfu tano zinazotumika kulipa wapishi na matumizi mengineyo nakwamba kwasasa wanafunzi wanamudu kukaa shuleni tangu asubuhi mpaka saa 11 jioni

Baadhi ya wanafunzi katika Shule ya Sekondari Gablanga wamewashukuru wazazi kwakukubali wapate chakula shuleni nakuwa afya zao zimeimarika ambapo awali walikuwa wakisinzia darasani kwasababu ya njaa,kutoroka shuleni kabla ya muda wakurudi nyumbani na wengine walikuwa na tabia yakuiba miwa kwenye na Matunda mengine kwenye mashamba ya watu kinyume na maadili

Sauti ya Baadhi ya wanafunzi wakielezea manufaa ya lishe shuleni

Shule 7 ambazo hazitoi huduma ya chakula cha mchana kwa wanafunzi katika Wilaya Missenyi ni Minziro, Rwemondo, Buyango,Gera,Bwanjai,Kikukwe na Kyaka