Kahama FM

KAHAMA:Bibi anamtafuta Bwana Nelson Bujaga amkabidhi kiwanja chake.

January 6, 2022, 12:17 pm

Bi Monica Athanas

Mkazi wa Bukondamoyo kata ya Muhungula Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga Bi Monica Athanas anawaomba wasamalia wema wanaomfahamu Bwana Nelson Samatini Bujaga au ndugu zake wamtafute ili aweze kuwakabidhi shamba la ukubwa wa robo tatu alilonunua Bwana Bujaga mwaka 2013 Manispaa ya Kahama.

Bi Monica ameiambia Kahama Fm kuwa yeye alikabidhiwa shamba na bwana Bujaga Mwaka 2015 ili alitunze kwa kulilima wakati bwana huyo alipomuaga kwenda Geita kutafuta maisha.

Ameongeza kuwa Bwana Nelson Samatini Bujaga alinunua shamba hilo kutoka kwa Bi Cristina Mpigi mwaka 2013 na vielelezo vyote anavyo na sahihi za mnunuzi na muuzaji pamoja na mashahidi wa pande zote.

Amesema tangu Bwana Bujaga aondoke hajawahi kurudi na kwamba mawasiliano ya simu aliyokuwa nayo kwasasa hayapatikani na kwamba imekuwa muda mrefu hivyo anamtafuta amkabidhi eneo lake ambalo alimkabidhi alitunze.

Sambamba na hayo Bi Monica amesema kuwa mara baada ya muuzaji wa shamba hilo kufariki baadhi ya viongozi wa mtaa kwa kushirikiana na mashahidi wa mauziano hayo wanataka kumgeuka na kulichukua shamba hilo jambo ambalo yeye amesema hawezi kulitoa kwa mtu yeyote.

Kufutia hatua hiyo Bi Monica ametoa taarifa kwenye ofisi ya Mkuu wa wilaya ambapo waliweka zuio kutoruhusu mtu yeyote   kufanya shughuli katika eneo hilo.

Mwishoni mwaka mwaka 2021 Bi Monica alienda Geita kata ya Nyamkumbu kumtafuta Bwana Nelson Samatini Bujaga bila mafanikio na kwamba kwa sasa hana uwezo wa kifedha kuzunguka kumtafuta bwana huyo.

Katika hatua nyingine Bi Monica ameiomba kamati ya Ulinzi na usalama ya wilaya kuingilia kati swala hili kwani yeye yuko peke yake na hana mtu wa kumsaidia.

Bi Monica amewaomba watanzania wote kwa mtu anayemfahamu bwana Nelson Samatini Bujaga au ndugu zake awasiliane naye kwa namba 0765-962812 au 0783-395398 ili aweze kuwapatia shamba lao.