kahama
Kahama FM

GEITA:Watoto wa Kituo cha Moyo wa Huruma waomba wasamalia kuwasaidia vifaa vya Shule.

January 1, 2022, 7:27 pm

Afande Joseph Kessy aliyesimama mwenye T-shrt Nyeusi akiwa na watoto wa kituo cha Moyo wa huruma Geita.

Watanzania wametakiwa kujitokeza kuwasaidia watoto wenye uhitaji hasa katika vituo vya watoto yatima vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwatia moyo na kuwafanya watoto hao wasijione wakiwa na wapweke katika jamii inayowazunguka.

Hayo yamesemwa leo na Msimamizi wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Moyo wa Huruma kilichopo mkoani Geita Sista Maria wakati akitoa neno la shukrani kwa Familia ya Afande Joseph Kessy ambaye ni msaidizi wa mkuu wa kituo cha Polisi Kahama aliyeandaa chakula cha mwaka Mpya kwa kituo hicho.

Maria amesema kuwa watoto waliopo katika vituo vya kulelea watoto yatima wanategemea huruma za wasalimia wema na mashirika mbalimbali hivyo watanzania wanapaswa kuwasaidia watoto hao kwani hawana watu wengine wa kuwasaidia zaidi ya wasamalia wema.

Sambamba na hayo ameongeza kuwa si lazima kutoa msaada wa vyakula wala pesa bali hata kuwatembelea na kuwaombea inawapa faraja na kwamba inawasaidia kuwajengea imani ya kuwa hawako peke yao.

Nao baadhi ya watoto wa kituo hicho wameishukuru familia ya Afande Joseph Kessy kwa kuwaandalia chakula na vinywaji katika sikukuu ya mwaka mpya na kwamba wamefurahia na wao wamesherehekea sikukuu kama watoto wengine walio baba na mama.

Watoto wa kituo cha Moyo wa Huruma wakipata chakula cha Pamoja na Familia ya Afande Joseph Kessy.

Katika hatua nyingine wamewaomba wasamalia wema kuzidi kuwasaidia hususan ni kuelekea katika muhula mpya wa masomo kwani wengi wao wanasoma na wanahitaji vifaa mbalimbali ikiwemo madaftari,Sare za shule,Kalamu pamoja na mabegi na viatu.

Kwa upande wake Joseph Kessy ameshukuru kupata nafasi ya kushiriki chakula cha sikukuu ya mwaka mpya na watoto hao pamoja na familia yake,Na kutoa wito kwa watanzania wengine kujitoa kwa hali na mali kuwasaidia watoto walio katika vituo vya kulele watoto yatima.

Kituo cha kulelea watoto yatima cha Moyo wa Huruma kinachopatikana Wilayani Geita mkoani Geita kina watoto wapatao 157 ikijumuisha watoto wa kike na wakiume.