dodoma
Kahama FM

DODOMA:Tumieni Teknolojia ya Internet kujikwamua Kiuchumi.

December 7, 2021, 6:49 pm

Wanachama wa Mitandao ya kijamii wametakiwa kutumia Teknolojia ya matumizi ya internet kujikwamua kiuchumi hususan katika maeneo ya pembezoni ikiwa ni pamoja na kuimarisha vikundi vya ushirika ili vitambuliwe na serikali na viweze kusaidiwa.

Wito umetolewa jana Jijini Dodoma na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania Bara Dkt Benson Ndiege wakati wa ufunguzi wa Toleo la pili la warsha ya wadau wa Shule ya usimamizi wa mtandao Jamii Tanzania.

Dkt Ndiege amesema kuwa mitandao ya kijamii imekuwa ni njia kubwa ya mawasiliano duniani kote inayorahisisha kukutana na kundi kubwa la watu kwa wakati mmoja na kupunguza gharama mbalimbali zikiwemo usafiri.

Sambamba na hayo Dkt Ndiege ametoa Pongezi kwa mwanzilishi wa wazo la Mtandao Jamii Tanzania Ndg. Jabhera Matogoro kwa kutambua umuhimu wa Mtandao katika jamii hasa za pembezoni na kutoa wito kwa mashirika na Taasisi mbali mbali kuunga mkono jitihada hizi.

Naye Mbunge wa Manyoni Mashariki Mheshimiwa Dkt. Pius Chaya ambaye alikuwa msemaji katika warsha hiyo amesema kuwa ili vyama vya ushirika vya Mtandao Jamii viweze kufanikiwa vinatakiwa kushirikisha mawazo kwa viongozi wa maeneo yao wakiwemo wabunge, wakuu wa wilaya na wakurugenzi ili wawasaidie kuyafikisha kwa watoa maamuzi na kuongezewa mawazo mapya.

Mbunge wa Manyoni Mashariki Mheshimiwa Dkt. Pius Chaya

Kwa upande wao baadhi ya wanachama wa vyama vya ushirika vya mtandao jamii kutoka Kondoa, Nyasa na Kasulu wameshukuru waandaaji wa mkutano huo kwa kuwakutanisha na watu mbali mbali kwani umewasaidia kutambua mambo mengi ambayo yatawasaidia katika shughuli zao za mitandao jamii.

Toleo la pili la warsha ya wadau wa Shule ya usimamizi wa mtandao Jamii Tanzania lililofanyika Dodoma limeshirikisha wadau 80 kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Zimbabwe, Afrika Kusini, India, Uingereza, Mauritius, Norway na Marekani.

Toleo hili la mwaka 2021 limeandaliwa na Tanzania Community Networks Alliance, Kondoa Community Network Cooperative Society Ltd, Kasulu Community Network Cooperative Society Ltd na Nyasa Community Network Cooperative Society Ltd na Limedhaminiwa na Internet Society, Association of Progressive Communications, Alliance for Affordable Internet, AFRINIC, TechSonic na Basic Internet Foundation.