job ndugai
Kahama FM

DODOMA:Job Ndugai azionya Asasi kuacha kutumika kuchafua nchi.

October 24, 2021, 11:02 am

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai, akifungua wiki ya AZAKI Jijini Dodoma.

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai, amefungua rasmi wiki ya Asasi za kiraia (AZAKI) Jijini Dodoma na kuzionya baadhi ya asasi kuacha kutumika kuchafua nchi.
Uzinduzi wa wiki hiyo ya Asasi za kiraia  umefanyika katika viwanja vya ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Ndugai amesema anatambua mchango mkubwa wa Asasi za kiraia hapa nchini, katika ukuaji wa maendeleo ya taifa na kuhudumia wananchi, na kuzitaka Asasi ambazo zinatumika vibaya kuichafua nchi na viongozi ziache mara moja.

“Serikali inatambua mchango wa asasi za kiraia hapa nchini, na tunaomba muendeleze miradi yenu kwa kutafuta fedha ndani na nje ya nchi, na kuzileta kwa ajili ya maendeleo ya Taifa,” alisema Spika Ndugai.

Aidha ,alisema asasi la kiraia zimekuwa zikifika maeneo ambayo Serikali haiwezi kufika, na kuwahudumia wananchi katika makundi mbalimbali kutatua changamoto zao, wakiwemo watu wenye ulemavu, yatima na wajane.

Katika hatua nyingine Ndugai alisema, Ofisi ya Bunge itaendelea kushirikiana na asasi za kiraia katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Umma Fredy Mwakibete ,ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Busekelo, akiwa katika Banda la HakiRasilimali, amezipongeza Asasi za kiraia, kwa kazi nzuri ambazo wanafanya hapa nchini.

Alisema kutokana na kazi hiyo nzuri, kuna haja ya Serikali kuangalia uwezekano wa kutenga fungu katika bajeti yake, na kuziwezesha Asasi za kiraia katika kuwahudumia wananchi.

Pia ameipongeza Taasisi ya HakiRasilimali, kwa kazi zao ambazo wanazifanya ya uziduaji katika Sekta ya Madini, Oil na Gesi, na hata kutoa elimu kwa wanawake zaidi ya 2,000 kushiriki katika Sekta ya madini.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya HakiRasilima Rachel Chagonja, alisema bado kuna changamoto ya masuala ya mila na imani potofu, juu ya wanawake kushiriki katika masuala ya uziduaji hasa Sekta ya madini, na kuiasa jamii iachane na mila hizo, ili kuleta usawa wa kijinsia katika uwajibikaji.

Wiki hii ni wiki ya Asasi za kiraia (AZAKI) hapa nchini, yenye kauli mbiu isemayo, “Azaki na Maendeleo” ambapo Spika wa Bunge Job Ndugai, kabla ya kuzindua, alitembelea mabanda mbalimbali ya Azaki, likiwemo la HakiRasilimali ambao wanajihusisha na masuala ya uziduaji kwenye Sekta ya madini, oil, na Gesi.