jafo
Kahama FM

SERIKALI:Wafanyabiashara marufuku kuuza majokofu na viyoyozi vya Mtumba.

September 17, 2021, 3:49 pm

Majokofu ya Mtumba

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Seleman Jafo amewataka wafanyabiashara kuacha kuuza Majokofu na Viyoyozi vya mtumba kwani vimeonekana kuleta athari kubwa katika vizazi vijavyo.  

Amebainisha hayo jijini Dodoma wakati alipokuwa akifanya ziara katika maduka na kwa fundi wanaojishughulisha na uuzaji na utengenezaji wa majokofu na viyoyozi katika maadhimisho yakupambana na kulilinda Anga la hewa (Ozone layer).

Amesema wafanyabishara wengi wamekuwa wakiuza majokofu yamtumba yalikuwa yakitumia gesi R22 ambayo yalikuwa yakiharibu mazingira ambapo bidhaa hizo zinazoletwa kutoka katika nchi za nje zimekuwa zikileta madhara makubwa katika Anga la hewa na kuwataka wafanyabishara hao kuuza mitungi ya gesi kuanzia R200 na kuendelea.  

“Majokofu ya mtumba yamekuwa yakiharibu mazingira na wananchi wamekuwa wakinunua, madhara yapo mengi endapo tutaendelea kuharibu anga la hewa (Ozone layer) kuna uwezekano mkubwa huko baadae kuzaa watoto wachanga wenye upofu na madhara mengine watu kubabuka ngozi,”amesema Waziri Jafo.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Seleman Jafo

Pia ametoa wito kwa vijana ambao ndio mafundi wanaojishughulisha na masuala ya ufundi wa viyoyozi kwenye Majokofu ya mtumba kutumia aina ya gesi iliyoruhusiwa.

Kwa upande wake fundi anayejishughulisha na Ufundi wa Viyoyozi Matukuta Juma amesema wao mafundi wanatumia mitungi ya gesi ya R22 iliyotambulika kama inaharibu mazingira kutokaa na unafuu ambapo ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuwapunguzia gesi ambayo haiharibu mazingira kwani inauwza bei ya juu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Remidius Mwema akimuakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amesema Dodoma inakuwa kwa kasi hivyo kuna haja ya kutengeneza jukwaa la pamoja litakalosaidia kutoa elimu kwa wananchi.

“Ni kweli wananchi wamekuwa wakinunua Majokofu ya mtumba ambayo yameonekana kuwa na madhara na hiyo yote inatokana na kutokuwa na uelewa juu ya madhara hayo lakini sasa kama tutakuwa na jukwaa la pamoja la kutoa elimu juu ya madhara ya bidhaa hizi za mtumba ninaimani bidhaa hizo za mtumba hazitanunuliwa,”amesema