Kahama FM

Shinyanga: serikali yaunda timu maalumu ya kupitia mfumo wa mauzo ya mazao ya dengu, choroko, mbaazi na ufuta.

September 16, 2021, 11:43 am

Waziri wa Kilimo Prof. Adolph Mkenda

Serikali imeunda Timu Maalumu ya Kupitia Mfumo wa Mauzo kwa mazao ya Jamii ya mikunde ikiwemo Dengu, Choroko, Mbaazi na Ufuta kwa ajili ya kusikiliza na kupokea maoni kwa wadau kuhusu namna bora ya kutekeleza ununuzi wa mazao hayo katika mfumo wa Stakabadhi ghalani ambao umeleta mivutano ikiwemo kuzuia na kuachia mazao ya dengu yaliyokuwa yanasafirishwa na wafanyabiashara.

Timu hiyo imetangazwa jana Jumatano Septemba 15,2021 na Waziri wa Kilimo Prof. Adolph Mkenda wakati wa Mkutano wake na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Prof. Mkenda amesema Timu hiyo itaongozwa na Mwenyekiti Dkt. Hamis Mwinyimvua aliyekuwa Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Nishati kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Katibu Bw. Ernest Doriye kutoka Wizara ya Kilimo na wajumbe ambao ni Dkt. Anaclet Kashuliza kutoka SUA, Dkt. Ruhinduka Remidius kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Bw. Barney Laseko kutoka Sekta Binafsi na Dkt. Wilhelm Ngasamiaku kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam pamoja na Wajumbe wa Sekretariati ambao ni Shaibu Chilavi na Samson Poneja.

Amesema kupitia Timu hiyo wadau ambao wana maoni kuhusu namna bora ya kufanya stakabadhi ghalani wataweza kutuma maoni yao na kwamba timu hiyo itakuwa na jukumu la kutengeneza vigezo gani vitumike kuamua zao flani liingie katika mfumo wa stakabadhi ghalani na utaratibu gani utumike kwa wakulima kupata fedha kabla ya mauzo halisi hayajafanyika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Timu Maalumu ya Kupitia Mfumo wa Mauzo kwa mazao ya Jamii ya mikunde ikiwemo Dengu, Choroko, Mbaazi na Ufuta, Dkt. Hamis Mwinyimvua amesema katika utekelezaji wa kazi yao watakahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwemo wakulima, wafanya biashara, viongozi wa serikali na vyama vya ushirika.

Naye Mkuu wa Mko wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati ameahidi viongozi wa mkoa watatoa ushirikiano mkubwa kwa timu hiyo ili kupata taarifa za msingi kuhusu maendeleo na changamoto ya mfumo wa manunuzi ya mazao jamii ya kunde ili waweke mapendekezo yatakayosaidia kuwa na msimamo wa pamoja ambao ni endelevu juu ya mfumo wa Stakabadhi ghalani.