TANESCO
Kahama FM

KAHAMA:Tanesco yatoa elimu maonyesho ya Biashara,Wananchi kunufaika na huduma.

August 28, 2021, 5:22 pm

Banda la TANESCO katika maonyesho ya Biashara Kahama.

Wananchi wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kutumia fursa ya uwepo wa maonyesho ya Biashara katika Manispaa hiyo  ili kupata elimu ya matumizi ya umeme na huduma za TANESCO ikiwa ni pamoja na kuuliza mambo wasiyoyafahamu kuhusu nishati hiyo.

Wito huo umetolewa leo na Afisa mahusiano na huduma kwa wateja wa shirika la Ugavi wa umeme TANESCO wilayani Kahama Jimmy Monyo wakati akizungumza na Kahama FM katika banda la Shirika hilo liliopo katika maonyesho ya biashara yanayoendelea wilayani Kahama.

Monyo amesema kuwa katika maonyesho hayo wameweka banda lao ambalo pamoja na kutoa elimu ya matumizi ya Umeme pia wanatoa fursa kwa wananchi kujaza fomu za awali za maombi ya maunganisho mapya ya umeme pamoja na kusikiliza kero mbalimbali.

Maonyesho ya Biashara Kahama,Hili ndilo banda la TANESCO.

Sambamba na hayo Monyo ameongeza kuwa katika banda hilo pia wanatoa elimu ya Kujikinga na athari za umeme,Elimu ya matumizi bora ya umeme (UMETA) pamoja na elimu ya Matumizi ya Mfumo wa Tanesco-(TANESCO APP).

Kwa upande wake Afisa Uhusiano na huduma kwa wateja mkoa wa Shinyanga Victoria Senge amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi ili kupata elimu ya umeme wa majumbani kwani wao ndiyo wanaoshinda muda mrefu na kutumia umeme mara kwa mara.

Maonyesho ya biashara Kahama yaliyobebwa na kauli mbiu Michezo,Afya na Biashara yameanza tangu August 23 na yanatarajia kuhitimishwa kesho August 29 na Mgeni rasmi Waziri wa habari utamaduni na Michezo Mh Innocent Bashungwa.