Kahama FM

ANAYEDAIWA KUWA JAMBAZI AFARIKI BAADA YA KUPIGWA RISASI SHINYANGA MJINI.

June 1, 2021, 6:29 pm

UBAKAJI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba

Mwanaume aliyejulikana kwa jina la Idd Masasi (43) anayedaiwa kuwa ni Jambazi amefariki dunia akipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga baada ya kupigwa risasi mguuni na mgongoni na askari polisi wakati akijaribu kuwakimbia katika Soko la Nguzo Nane Mjini Shinyanga.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari , Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema Mei 30,2021 Jeshi la polisi lilipata taarifa fiche za uwepo wa Jambazi aitwaye Idd Masasi mkazi wa Ndembezi Mjini Shinyanga na makazi mengine Kigamboni Jijini Dar es salaam.

“Mtuhumiwa huyo alikuwa anatafutwa kwa muda mrefu kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha hasa matukio yaliyotokea hivi karibuni Kigamboni jijini Dar es salaam. Taarifa fiche zilieleza kuwa jambazi huyo amekimbilia hapa Shinyanga baada ya kutenda matukio ya unyang’anyi jijini Dar es salaam hivi karibuni yenye namba KGD/IR/1050/2021 na KGD/IR/411/2021”,ameeleza Kamanda Magiligimba.

“Taarifa zilisema mtuhumiwa huyo anapenda kutembelea maeneo ya Soko la Nguzo Nane Manispaa ya Shinyanga kwa ajili ya kusoma maeneo ya kutenda uhalifu ikizingatiwa kuwa eneo hilo lina wafanyabiashara mbalimbali”,ameongeza.
Amebainisha kuwa kumbukumbu zinaonesha kwamba Idd Masasi alishawahi kuhukumiwa kufungwa miaka 30 kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha mwaka 2011 na kutumikia adhabu hiyo katika gereza la Butimba Mwanza na baadae alitoka kwa rufaa.

Amesema baanda ya Jeshi la polisi Shinyanga kupata taarifa hizo kwa kushirikiana na kikosi kazi cha askari polisi kutoka Dar es salaam, liliweka mtego maeneo ya Soko la Nguzo Nane na ilipofika majira ya saa tano asubuhi Mei 30,2021 Idd Masasi alifika maeneo hayo.

“Hata hivyo kikosi kabambe cha askari polisi wenye weledi mkubwa walikuwa tayari wameshamuona jambazi huyo na alipogundua kuwa anafuatiliwa jambazi huyo alianza kukimbia ndipo askari polisi walipompa ilani ya kusimama kwa kufyatua risasi hewani lakini hakusimama hivyo askari waliamua kumfyatulia risasi mbili kwa weledi wa hali ya juu bila kuleta madhara kwa watu wengine waliokuwepo eneo hilo……”.


“Risasi hizo zilimjeruhi jambazi huyo mguu wa kushoto na sehemu ya mgongoni na hivyo kuweza kumkamata. Jambazi huyo alikimbizwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu ya majeraha aliyoyapata na alifariki dunia wakati anapatiwa matibabu. Mwili wake umehifadhiwa hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi”,
amefafanua Kamanda Magiligimba.

Kamanda Magiligimba ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la polisi kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili mkoa wa Shinyanga uendelee kuwa salama.