Kahama FM

Vijana walionzisha kiwanda cha chaki Shinyanga walia kukosa soko.

April 15, 2021, 4:04 pm

Kikundi cha vijana 15 ambao ni wakazi wa Manispaa ya Shinyanga, walioanzisha kiwanda cha kutengeneza Chaki kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi, wamemuomba Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, kuwaunga mkono kwa kutoa maagizo kwa shule zote mkoani humo zinunue chaki kutoka kiwandani hapo.

Mwenyekiti wa kikundi hicho Hashimu Issa, akizungumza na Waandishi wa habari walipotembelea kwenye kiwanda hicho cha Chaki, amesema katika mkoa mzima wa Shinyanga wao pekee ndiyo wenye kiwanda cha Chaki, hivyo wanaomba uungwaji Mkono na Serikali ili wakue kiuchumi na kuchangia pato la Taifa.

Amesema kiwanda hicho walikianzisha mwaka jana, kupitia fedha za mkopo bila riba za Halmashauri asilimia nne za vijana Sh. Milioni 24.2 ili wajikwamue kiuchumi na kuendesha maisha yao kwa kujiajiri wenyewe, na kubainisha wanauwezo wa kuzalisha Chaki Boksi 30 kwa siku zenye  vipande 100 lakini hakuna soko la kutosha.

Aidha alisema kiwanda hicho kitakapopanuka, kitaongeza ajira nyingi kwa vijana tofauti na walivyo hivi sasa 15, na kuomba uugwaji wa mkono ili waendelee kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana mkoani Shinyanga.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, ambaye alitembelea kiwanda hicho hivi karibuni, aliwapongeza vijana hao na kutoa maagizo kwa walimu na wakuu wote wa Shule wilayani humo kununua chaki kiwandani hapo, huku akiahidi kuwatafutia masoko zaidi.