Kahama FM

Wawekezaji wa viwanda Shinyanga wapongeza maamuzi ya Rais Samia Kuhusu Kodi.

April 12, 2021, 6:57 am

BAADHI ya wawekezaji wa viwanda katika Manispaa ya Shinyanga mkoani hapa, wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassani kwa hotuba yake aliyoitoa hivi karibuni, wakati akiwapisha makatibu wakuu na manaibu kutoka wizara mbalimbali, na kuonyesha neema kwa wawekezaji hasa kwenye suala la ulipaji kodi.

Wafanyakazi wakiendelea na uzalishaji wa Pombe Kali katika Kiwanda cha Canon General Supplies LTD.

Wawekezaji hao wametoa pongezi hizo leo wakati wakizungumza na waandishi wa habari walipotembelea kwenye viwanda vyao, kikiwamo cha utengezaji wa Pombe Kali cha Canon General Supplies na uchakati wa mafuta ya kula cha Jeilong.

Akitoa pongezi hizo, Meneja Msaidizi wa Kiwanda cha Canon General Supplies Ltd, Lazaro Simoni, amesema kuwa Rais Samia ameonyesha matumaini makubwa kwa wawekezaji hapa nchini kwa kuonya matumizi ya nguvu kwenye udaiwaji wa kodi, bali itumika njia rafiki hali ambayo itasaidia kutofungwa kwa viwanda vyao, na kuendelea kulipa kodi kidokidogo hadi kumaliza deni.

Meneja huyo ameongeza kwa kueleza kuwa, mwaka jana  Serikali ilikifunga kiwanda chao kwa masuala ambayo yalikuwa yanazungumzika, lakini kwa sasa wamefunguliwa na tayari leo kimeanza tena uzalishaji, ambapo imewabidi kupunguza idadi ya wafanyakazi 400 kati ya 500 waliokuwa nao na kubakia na wafanyakazi 100 kutokana na kupunguza kasi ya uzalishaji hali iliyosababishwa na bidhaa zao kupotea sokoni kutokana na kifungo walichokutana nacho.

.Nao baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho akiwamo Ladslaus Dominic na Amina Shamte, wamesema masuala ya ufungiaji viwanda hayana afya hapa nchini, ikiwa vina sababisha upotevu wa ajira nyingi kwa vijana, na kuaza kuishi maisha magumu, na kutoa wito kwa Serikali pale penye changamoto wakae wazungumze.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Kiwanda cha Mafuta ya kupikia cha Jielong, Zhongjun Ji, amesema wanamuunga mkono Rais Samia kwa kurudisha matumaini kwa wewekezaji wakiwamo wa kigeni, ambapo walikuwa wameshakata tamaa kutokana na utumiaji wa mabavu katika kudai kodi.

Pia ametoa ushauri kwa Serikali kupitia wizara husika kupunguza mlolongo mrefu wa utaoji wa vibari vya kazi kwa raia wa kigeni wanaowekeza nchini, ili kuwapa fursa ya kufanya shughuli zao kwa uhuru.