SIMIYU
Kahama FM

Wachimbaji wadogo watinga ofisi za DC na mabango ya kumkataa mwekezaji.

April 9, 2021, 8:14 am

Mgogoro wa mara kwa mara kati ya wachimbaji wadogo na watu wanaopewa leseni za uchimbaji na tume ya madini katika mgodi wa Bulambaka ulioko katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu umeingia katika sura mpya.

Wachimbaji wakiwa nje ya ofisi ya Mkuu wa wilaya na Mabango.

Mgogoro huo umewalazimu wachimbaji wadogo kuandamana katika Ofisi ya Mkuu wa wilaya na mkuu wa Mkoa, huku wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe za kumkataa mwekezaji aliyepewa leseni ya uchimbaji kwenye mgodi huo.

Wakiongea na waandishi wa habari, wachimbaji hao wakiwemo wamiliki wa mashamba, wamesema wameamua kufanya maandamano ili kupaza sauti zao kwa viongozi wakuu wa taifa.

Wamesema kuwa hatua zilizotumika kupatikana kwa mwekezaji huyo, zimegubikwa na usiri mkubwa, huku wakitaja uwepo wa viashiria vya rushwa katika upatakanaji wake.

Hata hivyo wachimbaji hao wamesema kuwa, wamiliki wa mashamba katika mgodi huo kwa muda wa mwaka mzima, wamekuwa wakiangaikia wapate leseni yao kutoka tume ya madini licha ya kukamilisha taratibu zote za uombaji.

Mmoja wa wachimbaji hao Masunzu Mboje amesema kuwa mwekezaji huo baada ya kufika kwenye mgodi huo, aliwataka wamiliki washamba kusaini hati ya makubaliano kwa nguvu huku wengine akiwapatia pesa (rushwa) ili waweze kusaini.

Aidha wachimbaji hao wamesema mwekezaji huyo aliyepewa leseni, amekuwa na vitendo vya unyanyasaji, pamoja na wizi wa madini ambapo walieleza amewahi kukamatwa akitorosha mawe yenye madini.

Mkuu wa Wilaya Festo Kiswaga akiongea na wachimbaji hao, alisema kuwa Ofisi yake haitambui leseni hiyo na wala hawezi kuongea jambo lolote juu ya mgogoro huo kwa sababu alitoa maelekezo na yameshindwa kutekelezeka na ofisi ya madini mkoa.

Naye mwekezaji huyo Hussen Makubi akiongea na waandishi wa habari juu ya tuhuma hizo, amesema kuwa yeye na wenzake wanaounda kikundi cha Buruwadu 4 Mine ndiyo wamepewa leseni ya kuchimba kwenye mgodi huo.

Makubi amesema kuwa leseni hiyo amepewa kihalali na hakuna vitendo vya rushwa kama wachimbaji hao walivyodai, huku akiiomba serikali kuingilia kati kwani shughuli za uchimbaji zimesimama kwa sasa.

Hata hivyo alipotafutwa Ofisa Madini hakuweza kupatakana kwa haraka, kwani alikuwa kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na usalama mkoa kilichokuwa kikiendelea katika ofisi ya mkuu wa mkoa kujadili suala hilo.