Jamii FM

Polisi yamkamata “anayetuhumiwa” kuteka watoto Mtwara

14 August 2021, 16:22 pm

Na Gregory Millanzi

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limemkamata mtuhumiwa Jabiri Bakari (19) kwa tuhuma za uhalifu wa utekaji, ubakaji na kulawiti watoto baada ya kuwalaghai kwa njia mbalimbali na kufanikiwa kuondoka nao kwenda kwenye maeneo na kunzisha makazi ya muda akiwa na watoto hao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara kamishna msaidizi wa Polisi (ACP) Mark Njera akifafanua mbele za waandishi wa Habari

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara kamishna msaidizi wa Polisi (ACP) Mark Njera amesema, mnamo tarehe 25.06.2021 huko mtaa wa Mbae Mashariki Manispaa ya Mtwara Mikindani, mtoto mmoja wa kike mwenye miaka 8 alipotea akiwa anacheza na wenzake na baada ya siku tano alipatikana Mnazi Mmoja Mingoyo mkoani Lindi akiwa amefanyiwa vitendo vya kikatili na mwanaume mmoja aliyemchukua na kuishi nae ambae alitambuliwa kwa sura.

Katika tukio lingine Kamanda Mark Njera amesema, mnamo tarehe 08.07.2021 eneo la Mbae Mashariki Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani hapa, mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 7 alitoweka na kwenda kusikojulikana akiwa anaenda shule.

Kamanda Mark Njera ameongeza kuwa, tarehe 24.07.2021 saa tatu asubuhi alipatikana maeneo ya Mbae Mashariki na alipohojiwa alisema alifanyiwa ukatili wa kijinsia kwa kuchezewa sehemu za Siri na mwanaume mmoja ambae alimfahamu kwa sura ambae alimchukua na kuishi nae.

Katika tukio la tatu mnamo tarehe 06.08.2021 saa kumi na moja jioni eneo la kwa Father Liumbo mtaa wa Mbae Mashariki mtoto mmoja wa kike mwenye umri wa miaka 09 alichukuliwa na mtu mmoja mwanaume ambae alimfanyia vitendo vya kikatili na tarehe 07.08.2021 saa nane Mchana alipatikana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara ACP Mark Njera amesema, jeshi la Polisi lilifanya uchunguzi na ufatiliaji wa kina kuhusu matukio hayo na ikabaini kuwa , matukio hayo yalikuwa yakitekelezwa na mtuhumiwa mmoja kutokana na mbinu alizokuwa anazitumia za kuwalaghai watoto hao, kuwa aliwanunulia pipi na kuwapatia fedha na pia kuwatisha anapofanikiwa kuwa nao.

Kamanda Njera ameongeza kuwa, mtuhumiwa wa makosa yote matatu tayari ameshakamatwa na jeshi la Polisi na atafikishwa Mahakamani Mara tu upelelezi utakapokamilika.

Pia Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara linatoa onyo kali kwa wale wote wanaojihusisha na uhalifu wa unyanyasaji wa kijinsia na ukatili kwa watoto, kwani vitendo hivyo havikubaliki kwenye JAMII na yeyote atakayejihusisha na vitendo hivyo atakamatwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Kamanda ACP Mark Njera ametoa wito kwa wananchi wote Mkoani Mtwara kuwa kila mmoja atambue kuwa jukumu la kuhakikisha ulinzi na usalama kwa watoto ni jukumu la malezi ya kila mmoja watu pia wananchi watoe taarifa Polisi kwa matukio na endapo kuna mtu wanamtilia mashaka Mitaani kwao.