Jamii FM

Mwenendo wa Kimbunga “JOBO”

24 April 2021, 06:33 am

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga “Jobo” kilichopo bahari ya Hindi. Kimbunga Jobo kimeendelea kusogea kuelekea maeneo ya pwani ya nchi yetu ambapo kutokana na taarifa za uchambuzi zilizofanywa na Mamlaka kimbunga Jobo kinasafiri kwa kasi ndogo ya kilometa 6 kwa saa ukilinganisha na kasi ya kilometa 12 kwa saa ya awali. Hali hiyo inatarajiwa kusababisha kimbunga Jobo kuingia nchi kavu katika nyakati za mchana Jumapili tarehe 25/04/2021.

Mwenendo wa Kimbunga jobo

Hali ya kupungua kwa kasi ya kimbunga “Jobo” inayojitokeza inaweza kuongeza viwango vya mvua katika maeneo kitakapopita kimbunga hicho. Vipindi vya upepo mkali unaofikia kilometa 50 hadi 60 kwa saa, mawimbi makubwa baharini pamoja na mvua kubwa kwa maeneo ya ukanda wa pwani vinatarajiwa kwa tarehe 24 na 25 ya mwezi Aprili, 2021.

Maeneo yanayotarajiwa kupata athari za moja kwa moja kutokana na kimbunga Jobo ni pamoja na mikoa ya Pwani (ikiwemo kisiwa cha Mafia), Lindi, Tanga, Dar es Salaam pamoja na kisiwa cha Unguja. Aidha, maeneo mengine yanayotarajiwa kuathirika ni mkoa wa Mtwara pamoja na kisiwa cha Pemba. Hata hivyo, izingatiwe kuwa uwepo wa kimbunga Jobo unatarajiwa kuendelea kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na kusababisha ongezeko la vipindi vya mvua kwa maeneo mengine hata yaliyo mbali na ukanda wa pwani (ikiwemo ukanda wa Ziwa Victoria).

USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.