Jamii FM

Kauli ya Rais imetupa nguvu mpya

18 April 2021, 10:28 am

Na Karim Faida.

Wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali kutoka kwenye soko kuu la Chuno lililopo manispaa ya Mtwara mikindani mkoani Mtwara wamesema wanaimani kubwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kutokana na kauli zake anazozitoa katika hutuba mbalimbali kwa watanzania.

Rose Sanga mfanyabiashara wa mbogamboga

Akiongea na Jamii fm radio jana Sokoni hapo Bi Rose Sanga mfanyabiashara wa mbogamboga na mkazi wa mtaa wa Sabasaba mkoani hapa amemuomba Mh Rais kuwaangalia zaidi Wafanyabiashara wadogowadogo kwa kuwa biashara hizo ndizo zinazowasaidia kuendesha maisha yao.

Nae Selemani Mtetemo ambaye ni mfanyabiashara wa ndizi katika soko hilo amesema soko lao ni kubwa na linakusanya watu wengi ambao wana ajira ndogondogo kama vile Mama ntilie, wauzaji wa matunda na mbogamboga, wazoa taka, walinzi na wengine hivyo kuendelea kuwapambania Wafanyabiashara hao hasa kwenye swala la ushuru kama alivyozungumza mwenyewe itasaidia kuongeza idadi ya wafanyabiashara sokoni hapo na hivyo uchumi kupanda.

Hotuba iliyowagusa Wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla ni ile aliyoitoa Jumanne ya April 6 2021 Ikulu Jijini Dar es salaam katika hafla ya kuwaapisha Makatibu na manaibu wa wizara mbalimbali ambapo aliagiza kusimamia swala la kodi kwa wafanyabiashara na kutowabana sana maana wanaweza kufunga biashara na kuhamia Nchi zingine.

Soko la Chuno ni soko kuu jipya lililozinduliwa Desemba 25 2020 na aliyekuwa Waziri Ofisi ya Rais tawala za mikoa na Serikali za mitaa TAMISEMI Selemani Jafo na limegharimu Tsh bilioni nne na milioni mianane.