Jamii FM

Njia yenye mawe yawakimbiza wanafunzi wa kijiji cha Imekuwa

24 March 2021, 11:24 am

Wananchi wa kitongoji cha Bohari pwani kilichopo kwenye kijiji cha Imekuwa halmashauri ya wilaya ya Mtwara mkoani hapa wamekubaliana kuwaondoa watoto wote wenye umri wa kuanza shule katika kitongoji hicho na kuwapeleka kwenye kijiji cha Imekuwa ili waweze kupata elimu.

Akiongea na Jamii fm radio baada ya kuwatembelea kitongojini hapo siku ya Februari 08, 2021 Hamisi Malatu mmoja kati ya wakazi wa muda mrefu wa eneo hilo amesema sababu inayopelekea kuwaondoa watoto hao ni kuwepo kwa mawemawe kwenye njia inayotumika kufika eneo hilo hivyo kwa watoto hawawezi kuitumia.

Malatu amesema ukiwa unatembea kwenye njia hiyo inataka umakini mkubwa maana ukiteleza ni rahisi kuumia hivyo hawakuona sababu ya kuishi na watoto ambao pengine wasingefurahia masomo kutokana na adha hiyo. Watoto hao hupelekwa kwa ndugu zao na wengine wanaishi na mama zao katika makazi yao huku akina baba wakisalia kwenye kitongoji hicho kwa shughuli za uvuvi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kitongoji hicho Ismaili Mtunduka amesema Elimu ni muhimu kwa kila mtu hivyo uamuzi wa kuwaondoa watoto wenye umri wa kwenda shule wamekubaliana wananchi wote.

Mtunduka ameongeza kuwa ni rahisi kwa wananchi kukubaliana jambo hilo kwa kuwa wakazi wengi wa kitongoji hicho wana nyumba zao katika kijiji cha Imekuwa ambapo ndipo pana shule ya msingi. Kitongoji hicho kipo tangu miaka ya 1940.

hali halisi ya barabara ianayotumiwa na wanafunzi kuelekeaa shuleni