Huheso FM

HABARI ZA SENSA ZITOKE KWENYE VYANZO SAHIHI

June 17, 2022, 12:46 pm

Wahariri wa vyombo vya habari vya Redio jamii wameombwa kuhakikisha wanashiriki zoezi la sensa kwa weledi kwa kutoa taarifa za habari zenye vyanzo sahihi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Hayo yamesemwa na muwasilisha mada Dkt. Abubakar Rajab katika mafunzo ya wahariri wa redio Jamii yaliyoandaliwa na Taasisi ya Tanzania Development Information Organization (TADIO) kwa ushirikiano na ofisi ya takwimu ya taifa (NBS) yanayofanyika katika chuo kikuu Cha Mkwawa mkoani Iringa.

Amesema wahariri wa redio Jamii wanayo nafasi kubwa ya kuifikishia Jamii taaeifa sahihi zinazokusanywa na wandishi wao kutoka vyanzo sahihi ambavyo Jamii itaweza kuhamasika na kushiriki kikamilifu zoezi la sensa.

Nae afisa habari kutoka ofisi ya taifa ya takwimu (NBS) Bw. Said Amir amesema wahariri kwa kushirikiana na wandishi wao wanaoandika habari zinazohusu sensa wanapaswa kuwa karibu na wataalam wa masuala ya sensa ili kupata habari zenye uhakika.

Aidha mtaalam wa idadi ya watu Bi. Hellen Siriwa amesema siku ya zoezi la sensa litakapowadia Kila mwananchi atahesabiwa ili kupata idadi kamili ya watu kwenye maeneo yao na taifa kwa ujumla huku akiongeza kuwa hata watu watakaokuwa wameshikiliwa katika vituo vya Polisi, Mahabusu, kulazwa hospitali wote watafikiwa kwa ajili ya kuhesabiwa.

Hata hivyo mafunzo ya sensa kwa wahariri wa vyombo vya habari (Redio Jamii) yamefungwa leo ambayo yamefanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia Juni 16-17, 2022 katika chuo kikuu cha Mkwawa, Manispaa ya Iringa mkoani Iringa.