Huheso FM

Wananchi wamlalamikia mwenyekiti wa mtaa wao

May 18, 2021, 5:54 pm

Wananchi wa Mtaa wa Bulima Kata ya Seeke Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wamemlalamikia mwenyekiti wa mtaa huo kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa wananchi hivyo wamemtaka kujiuzulu mara moja.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika mtaani hapo wananchi hao wamesema wamekuwa wakimuomba kuhudhuria mikutano ya hadhara lakini amekuwa hatokei na kudai kuwa ana shughuli zake ambazo zinamfanya kutokuhudhuria mikutano hiyo.

Wamesema katika mkutano uliofanyika leo ulikuwa na lengo la kumtaka mwenyekiti huyo kuwasainia barua yao kuruhusiwa kufanya tambiko la kimila lakini amewakatalia na kuficha Mihuri ya kijiji hivyo kwa sasa hawamtambui na hapaswi kuendelea kushika wadhifa huo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Mtaa huo wa Bulima, Grace Nkuba amesema mkutano wa wananchi uliofanyika leo haukuwa rasmi hivyo hakuweza kuhudhuria kutokana na mkutano huo kuandaliwa kwa lengo la kujadili ni namna gani ya kuwafichua wachawi katika mtaa huo kitu ambacho hawezi kukubaliana nacho.

Hata hivyo wananchi hao wamesema wamekuwa hawaridhishwi na utendaji kazi wake kutokana na kutokuwa karibu na wananchi wa mtaa huo hali ambayo wamekuwa wakihangaika namna ya kupata huduma za kiserikali.