Huheso FM

FADEV kutoa ruzuku kwa wanawake Wachimbaji Wadogo wa Madini Shinyanga.

March 25, 2021, 2:37 pm

Katibu Mtendaji wa Taasisi ya kuendeleza FADev Tina Mwasha, akielezea malengo ya taasisi hiyo

TAASISI ya kuendeleza wachimbaji wadogo wa madini hapa nchini (FADev), wanatarajia kuanza utoaji wa fedha za Ruzuku kwa wanawake ambao ni wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu mkoani Shinyanga, pamoja na kuwapatia mkopo wa vifaa vya uchimbaji bila riba, ili kuwakuza kwenye sekta hiyo na kuwainua kiuchumi.

Meneja miradi kutoka tasisi hiyo Evance Lubara, alibainisha hayo jana wakati wakitambulisha mradi wa Jinsia kwenye sekta ya madini, wa kuwezesha wanawake kushiriki kikamilifu kwenye uchimbaji wa madini, ambao utatekelezwa mkoani Shinyanga, kwa kuanza na migodi iliyopo Msalala wilayani Kahama.

Alisema katika mradi wao wa jinsia, wamejipanga kuwawezesha wanawake kuwaunga kwenye vikundi vya ujasiriamali ambao ni wachimbaji wadogo, na kisha kuwapatia fedha ili wapate mitaji ya kuendesha shughuli hizo za uchimbaji madini, pamoja na vifaa vya uchimbaji bila riba na kuinuka kiuchumi.

“Taasisi yetu ya FADev tumeanza kuwezesha wanawake ambao ni wachimbaji wadogo wa madini, kuwapatia fedha za Ruzuku kwa ajili ya mitaji, ambapo tuta anza na kuwezesha kutoa kiasi cha fedha Sh. 500,000 hadi Milioni moja kupitia kwenye vikundi, na watakao kuwa wakifanya vizuri wataongezewa Ruzuku,” alisema Lubara.

Aidha alisema pia vikundi hivyo vya wanawake wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu, watakuwa wakikopeshwa vifaa vya kisasa vya uchimbaji madini bila ya kutozwa riba, lengo likiwa ni kuwainua akina mama kwenye sekta hiyo ya madini na kiuchumi.

Kwa upande wake Katibu mtendaji wa Taasisi hiyo ya FADev, Tina Mwasha, alisema katika mradi huo, watawapatia pia wanawake elimu ya ujasiriamali, wakiwamo na wanaume, ili fedha wanazozipata waziwekeze kwenye miradi mingine ya maendeleo na kukua kiuchumi, ikiwa ipo siku madini yataisha au wao kumaliza nguvu za uchimbaji.

Mwasha alisema mbali na kuwezesha wanawake, pia watakuwa wakitoa elimu kwa wachimbaji wote wadogo wa madini, namna ya utunzaji wa mazingira, usalama kwa kuvaa vifaa kinga, kuacha matumizi ya kemikali, pamoja na kutunza taarifa za mauzo ya madini, ili wakopesheke kwenye taasisi za kifedha.

Naye Ofisa maendeleo ya jamii mkoani Shinyanga Tedyson Ngwale, alisisitiza kwenye uwezeshaji huo wanawake wachimbaji wadogo wa madini, wapewe zaidi vifaa vya uchimbaji madini kuliko fedha, ili kuondoa changamoto ya ulaji fedha hizo za Ruzuku.

Pia Katibu wa chama cha wachimbaji wadogo wa madini mkoani Shinyanga (SHIREMA) Gregory Kibusi, alisema taasisi hiyo imefika katika muda muafaka, ambapo wachimbaji wadogo wanakabiliwa na changamoto nyingi wakiwamo wanawake, ambao wamekuwa wakikosa haki zao sababu ya masuala ya mifumo kandamizi zikiwamo mila na mfumo dume.