Dodoma FM

UVCCM kuitangaza Kongwa

30 June 2023, 3:43 pm

Makamu mwenyekiti wa UVCCM Taifa bi Rehema Sombi pamoja na mbunge wa Jimbo la Kongwa Mheshimiwa Job Ndugai wakipata elimu ya historia ya wapigania uhuru wa nchi za Afrika Katika ukumbi wa veta Kongwa. Picha na Bernadetha Mwakilabi

Amesema jumuiya ya vijana ni tegemeo kwa chama inaweza kuleta vuguvugu la maendeleo hivyo kama vijana wanahakikisha wanakuwa na maadili mshikamano na mahusiano mazuri kwa Chama na Serikali.

Na Bernadetha Mwakilabi.

Makamu mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa bi Rehema Sombi amewataka vijana nchini kutembelea kujifunza na kuitangaza historia ya wapigania uhuru iliyopo wilayani Kongwa.

Bi Sombi ameeleza hayo alipotembelea wilayani Kongwa Katika Kambi za wapigania uhuru wa nchi za Afrika akiwa ameambatana na wajumbe wa baraza kuu la UVCCM Taifa ili kuona na kujifunza historia ya maeneo hayo ambapo ameeleza kuwa kuna haja ya Serikali kutenga bajeti kwaajili ya kukarabati maeneo hayo ili historia isipotee.

Pia Sombi ameeleza kuwa watatafuta wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza kwa wingi wilayani Kongwa ili kusaidia kutangaza maeneo muhimu ya kihistoria kwani uchumi imara ni nguzo kwa siasa za taifa letu.

Nae Mbunge wa Jimbo la Kongwa Mheshimiwa Joab Ndugai ameeleza kuwa Kongwa imejengwa kwa historia ya mkoloni kwani hata mitaa yake mingi bado ina majina yenye asili ya kikoloni kama uhindini usomalini Morisheni nk

Ndugai amewataka vijana kushika elimu yaani kujiendeleza kujua mambo mengi zaidi wapambane kuhakikisha nchi inakuwa kiuchumi kwani umasikini ulifanya tudharauliwe na mataifa yaliyotutawala.

Makamu mwenyekiti wa UVCCM Taifa bi Rehema Sombi pamoja na wajumbe wa baraza kuu la UVCCM Taifa katika Kambi ya wapigania uhuru Kongwa sekondari. Picha na Bernadetha Mwakilabi.

Aidha mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya na Diwani wa Kata ya Kongwa Mheshimiwa White Zuberi akitoa elimu ya historia ya wapigania uhuru amesema amani na maendeleo tuliyonayo ni kutokana na harakati za ukombozi zilizofanywa na waasisi wetu huko nyuma.

“Vijana cha maana ni uzalendo lazima muipende nchi yenu” alisema Zuberi.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya Kongwa Mheshimiwa Remidius Mwema Emmanuel amefafanua kuwa historia ya Kongwa ilianza mwaka 1942 lakini historia ya ukombozi wa bara la Afrika ilianza 1958-1960 wakoloni wakifanya kilimo Cha karanga na kuongeza kuwa ni vyema vijana kufahamu historia ya nchi na mchango wa nchi yetu kwa mataifa mengine.

Mwema ametaja maeneo ya kihistoria yanayohitaji kuhifadhiwa wilayani Kongwa kuwa ni pamoja na shule ya sekondari Kongwa kwenye kambi ya wapigania uhuru, eneo la makaburi ya wapigania uhuru, eneo lililotumika Kwa mazoezi ya kulenga shabaha la Mdinde na uwanja wa ndege.

Vilevile Mwema ameeleza kuwa kuna mikakati mbalimbali ambayo wilaya kwa kushirikiana na Wizara ya Sanaa utamaduni na michezo inachukua katika kuhifadhi maeneo hayo ikiwemo kuyatangaza zaidi, kuyatambulisha kisheria na kufanya makongamano kwani “Kongwa mbeleko ya ukombozi wa Afrika”

Mbali na hayo ziara hiyo ya makamu mwenyekiti wa UVCCM Taifa imekuja siku chache baada ya ziara ya katibu mkuu wa Chama Cha mapinduzi CCM Taifa ndugu Daniel Chongolo wilayani humo alipotembelea maeneo ya wapigania uhuru wa nchi za Afrika ambapo Chama kimeona ni vema vijana wakajifunza ili kujua harakati za ukombozi wa bara la Afrika.