Dodoma FM

NIDA, shirika la Posta waingia ubia usambazaji vitambulisho

5 June 2023, 6:16 pm

Said Hamad Afisa usajili NIDA wilaya Kongwa akisoma taarifa. Picha na Bernadetha Mwakilabi.

NIDA imeingia ubia na shirika la Posta katika zoezi la usambazaji wa vitambulisho.

Na Bernadetha Mwakilabi.

Wananchi wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya vitambulisho vya taifa (NIDA) ikiwa ni njia pekee ya kufanikisha lengo la serikali la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wake.

Hayo yameelezwa na mkuu wa wilaya Kongwa Mheshimiwa Remidius Mwema Emmanuel alipokuwa kata ya Kibaigwa akizindua zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya taifa (NIDA) katika wilaya ya Kongwa ambapo ametoa siku saba kwa watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha wanawapatia vitambulisho wananchi wote ambao wapo kwenye orodha.

Kwa upande wake meneja wa udhibiti na usambazaji wa vitambulisho vya taifa makao makuu Bi Balbina Mtui amewataka wananchi kutambua kuwa kitambulisho cha taifa ni nyara ya serikali hivyo kitumike na mtu mmoja na si vinginevyo.

Pia Bi Mtui amefafanua kuwa wananchi wenye namba za utambulisho wa taifa wanaosubiri vitambulisho hivyo wataendelea kupata huduma zote muhimu.

Pichani wananchi wakiwa katika hafla fupi ya kuzindua ugawaji wa vitambulisho vya Taifa NIDA.Picha na Bernadetha Mwakilabi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na afisa msajili wa vitambulisho vya taifa wilayani Kongwa Bwana Said Hamad jumla ya namba za vitambulisho vya taifa 120,702 zilizozalishwa wilayani Kongwa kati yake vitambulisho 100,334 vimekamilika  sawa na 83% tangu kuanza kwa mpango huo.

Bwana Hamad ameeleza kuwa katika zoezi hilo jumla ya wananchi 65,334 kati ya 120,702 waliojiandikisha watapatiwa vitambulisho huku zoezi la kuwasajili wateja wapya likiendelea.

Mwema akikabidhi kitambulisho Cha Taifa NIDA Kwa mmoja wa wananchi wa Kibaigwa Kongwa.

Akizungumza kwa niaba ya menejimenti ya shirika la Posta Bwana Stephen Kibona amesema kuwa mamlaka ya vitambulisho vya taifa NIDA imeingia ubia na shirika la Posta katika zoezi la usambazaji wa vitambulisho na kupitia mfumo wa anwani za makazi shirika litawafikishia hadi mahali walipo.