Dodoma FM

Mnada wa kisasa nyama choma kukuza uchumi wa wafanyabiashara

2 June 2023, 1:44 pm

Picha ni eneo ambalo litatumika kwa ajili ya mnada huo wa nyama choma Mbande wilayani Kongwa. Picha na Bernadetha Mwakilabi.

Na Bernadetha Mwakilabi.

Halmashauri ya wilaya ya Kongwa inatarajia kuanzisha mnada mpya wa kisasa wa nyama choma katika eneo la Mbande utakaosaidia kukuza uchumi wa wafanyabiashara na kuitangaza wilaya hiyo kibiashara.

Hayo yamesemwa na mjumbe wa kamati ya maandalizi ya mnada wa kisasa wa nyama choma Bi Sifras Nyakupora alipokuwa akitoa taarifa fupi ya mpango kazi wa kamati hiyo mbele ya mkuu wa wilaya Kongwa walipotembelea kukagua eneo lililotengwa kwa ajili ya mnada huo katika kijiji cha Mbande ambapo ameeleza kuwa mnada huo utasaidia kuwakusanya pamoja wafanyabiashara wa nyama choma wakubwa na wadogo.

Sauti ya mjumbe wa kamati ya maandalizi ya mnada .

Aidha Bi. Nyakupora ameongeza kuwa mnada huo utakuwa chachu kwa maeneo ya Kongwa na nje ya Kongwa kwani kwa tathmini yao hakuna wilaya ya jirani iliyoweza kuwa na biashara kama hiyo.

Sauti ya mjumbe wa kamati ya maandalizi ya mnada .

Amesema mara baada ya kuanzishwa mnada huo utakuwa ukifanyika kila siku za Jumapili na utajumuisha karibia nyama choma za wanyama wa aina mbalimbali wakiwemo kuku, bata, ng’ombe, mbuzi na kondoo.

Sauti ya mjumbe wa kamati ya maandalizi ya mnada .
Viongozi wa wialaya ya Kongwa wakikagua eneo hilo. Picha na Bernadetha Mwakilabi.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya Kongwa Mheshimiwa Remidius Mwema Emmanuel amesema ili mnada huo uweze kufanikiwa unahitaji nguvu ya halmashauri, serikali na wadau wa biashara ya nyama choma hivyo kila mmoja mwenye nafasi anaruhusiwa kushiriki katika fursa hiyo ya maendeleo kiuchumi.

Sambamba na hayo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Kongwa Dkt. Omary Nkullo ameitaka kamati ya maandalizi ya mnada huo kuweka mpangilio mzuri kwa kuzingatia mazingira ya eneo halisi na afya za walaji hivyo kila biashara ikae katika eneo lake ili kusaidia wateja kujua ni eneo gani inapatikana huduma fulani.