Dodoma FM

DUWASA watangaza utiaji saini wa mkataba wa Mradi wa kuboresha na kutibu maji taka

10 May 2023, 6:17 pm

Mradi huu unategemewa kuongeza huduma ya majitaka kutoka asilima 20 ya sasa hadi 45.Picha na Seleman Kodima.

Gharama za mradi wa Usanifu na Ujenzi  WA UBORESHAJI HUDUMA YA UONDOSHAJI NA KUTIBU MAJITAKA  unategemea kugharimu Dola za Marekani milioni  (70) sawa na Shilingi za Tanzania bilioni 164.85.

Na Selemani Kodima.

Katika kukabiliana na ufanisi  mdogo wa miundombinu ya kuondosha na kutibu majitaka  katika jiji la Dodoma ,Hatimaye Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Dodoma (DUWASA) leo wametangaza utiaji saini wa   Mkataba wa Usanifu na usimamizi wa ujenzi wa MRADI WA KUBORESHA HUDUMA YA UONDOSHAJI NA KUTIBU MAJITAKA na Mhandisi Mshauri Kampuni ya DOHWA .

Utiaji saini huo umefanyika jijini Dodoma katika ofisi za DUWASA ambapo Mradi huu unalenga kuhusisha usanifu na ujenzi wa mabwawa mapya makubwa 16 yenye uwezo wa kutibu takribani lita milioni 20 kwa siku, usanifu na ujenzi wa bomba kubwa (trunk main) kwa kilomita 107.5, ubadilishaji (replacements) wa bomba chakavu kilomita 2.6 na ukarabati (renovation) wa kilomita 2.1 za mtandao wa majitaka.

Akizungumza baada ya zoezi la utiaji saini kufanyika Waziri wa Maji Mhe Juma Aweso  amesema kuwa moja eneo ambalo hawajafanya uwekezaji mkubwa ni pamoja na eneo la majitaka hivyo

Amesema ujenzi wa mradi huo utaanza na hatua ya usanifu na usimamizi wa ujenzi ambapo umegharimu kiasi cha cha Dola za Marekani 5,225,000 sawa na takribani Shilingi za Kitanzania Bilion 12.3.

Sauti ya Waziri wa maji.

Aidha Waziri wa Maji Mhe Aweso amesema kuwa jukumu lao ni kuhakikisha wanausimamia mradi huo na kuhakikisha usanifu unakamilika kwa wakati.

Kwa upande wake Katibu mkuu wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa  Kemikimba amesema hatua waliofikia leo ya utiaji wa saini mkataba huo ni hatua iliyosubiriwa  hasa kwa mkoa wa Dodoma .

Picha ni mikataba ya mradi huo ambayo tayari imetiwa saini.Picha na Selaman Kodima.

Mhandisi Kemikimba amesema kuwa miezi 13 ambayo imetolewa kwa Mhandisi Mshauri Kampuni ya DOHWA inatakiwa itekelezwa kwa wakati ili inapokamilika na mkandarasi kupatikana kazi iweze kuanza mara moja.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph akisoma taarifa ya Mradi huo amesema chimbuko la mradi huo ni Kutokana na ongezeko la watu baada ya Serikali kuhamia jijini Dodoma, miundombinu ya kuondosha na kutibu majitaka kuwa  finyu na isiyotosheleza.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira

Aidha Mhandisi Aron amesema kuwa Ili kutatua tatizo hilo Serikali kupitia mpango wa maendeleo ya sekta ya Maji, ilipendekeza kuongeza na kuboresha mtandao wa kukusanyia na kusafirishia majitaka na  ujenzi wa mabwawa mapya makubwa ya kutibu majitaka katika Jiji la Dodoma.