Dodoma FM

Wakazi wa Chamwino watakiwa kutunza miundombinu ya maji

25 April 2023, 5:53 pm

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma katika picha akizindua mradi huo wa maji wilayani Chamwino. Picha na Seleman Kodima.

Itakumbukwa kuwa Mwaka 2020 jiwe la msingi la Mradi huo liliwekwa ikiwa ni ishara ya kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa tenki la maji Buigiri ambapo April 25 Mwaka huu .

Na Seleman Kodima.

Ikiwa leo ni maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,Mkoa wa Dodoma umeadhimisha siku hii kwa Uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi maji  ujazo wa lita milioni 2.5 ambapo itasaidia kuongeza hali ya upatikanaji wa maji katika wilaya ya Chamwino kwa Asilimia 45.

Akizindua mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule amesema kuwa mkoa wa Dodoma unakua kwa kasi hivyo ni muhimu ukuaji huo uende sambamba na upatikanaji wa maji ya kutosha katika kila eneo .

Aidha amewataka wananchi wilayani Chamwino kuhakikisha wanatumia vyema maji hayo hasa kwa kutunza miundombinu ya maji,Vyanzo vya maji ili kuwezesha shughuli nyingine kufanikiwa kupitia upatikanaji wa maji wilayani humo.

Kwa upande wake Katibu mkuu wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Sadiki Kemikimba amesema mradi huo utawezesha upatikanaji wa maji kwa wakati kwa wakazi wa chamwino na kupunguza matatizo ya kiafya yanayosababisha na changamoto ya maji.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Duwasa Mhandisi Aron Joseph akitoa taarifa mbele ya mkuu wa mkoa wakati zoezi la uzinduzi wa mradi huo amesema kuwa

Mradi huo umesimamiwa na Duwasa   katika hatua za manunuzi ya vifaa vya ujenzi huku zoezi la ujenzi likitekelezwa na Suma Jkt  na kukamilika kwa mradi huo ni muendelezo wa mkakati wa kuongeza hali ya upatikanaji wa maji katika wilayani ya Chamwino.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma pichani akiwa na viongozi mbalimbali akiwemo katibu tawala wa Mkoa wa Dodoma wakiti akizindua mradi huo. Picha na Seleman Kodima.

Baadhi ya wananchi ambapo wameshiriki katika Uzinduzi huo wamesema uzinduzi wa tenki hilo la maji ni moja ya hatua kubwa ya kuendelea kumaliza tatizo la maji katika wilaya ya Chamwino  na wanategemea kusahau madhila waliyowahi kupitia kutokana na umbali wa upatikanaji wa maji safi na salama.

Hatimaye uzinduzi wa mradi huo umefanikiwa huku Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira mkoa wa Dodoma DUWASA Wakiendelea kutatua changamoto ya maji pembezoni mwa jiji la Dodoma .