Dodoma FM

Wananchi wilayani Bahi wasisitizwa kulima mtama

13 March 2023, 3:43 pm

Mkuu wa wilaya ya Bahi Mheshimiwa Godwin Gondwe akisisitiza wananchi wa wilaya hiyo.Picha na Benard Magawa

Mheshimiwa Godwin Gondwe amewaagiza wananchi wilaya ya Bahi kuhakikisha kila kaya inalima ekari mbili za mtama ili kuepuka adha ya kukosa chakula.

Na Benard Magawa.

Mkuu wa wilaya ya Bahi Mheshimiwa Godwin Gondwe amewaagiza wananchi wilayani humo kuhakikisha kila kaya inalima ekari mbili za mtama ili kuepuka adha ya kukosa chakula kwa kulima mazao yasiyostahimili ukame kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yanayoikumba Dunia kwa sasa.

Mheshimiwa Gondwe ameyasema hayo kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Bahi sokoni mwishoni mwa wiki iliyopita ukishirikisha kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo pamoja na wakuu wa idara na taasisi zote za serikali wilayani Bahi ukilenga kusikiliza na kutatua kero za wanachi.

Akielezea kuhusiana na kuanzishwa kwa kilimo hicho Mheshimiwa Gondwe amesema Mazao kama mtama na alizeti yana wateja wa kutosha hivyo yanaweza kuwakwamua wananchi kiuchumi kwani tayari wilaya imefanya mazungumzo na shirika la chakula duniani (WFP) wamekubali kununua mtama kutoka Bahi.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Bahi Mheshimiwa Godwin Gondwe.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi wilaya ya Bahi SSP Ibrahim Idd Abdala ameeleza hali ya usalama ilivyo katika wilaya hiyo kwa kusema kuwa hali ya usalama ni nzuri na hakuna matukio yoyote ya ujambazi ndani ya miaka mitatu.

Kamanda wa Polisi wilaya ya Bahi SSP Ibrahim Idd Abdala akieleza hali ya usalama ilivyo katika wilaya hiyo.Picha na Benard Magawa

“Nawashukuru wazazi kwa kuwalea vizuri vijana wenu lakini baadhi siyo wote, miwasihi wananchi kuepuka kabisa vitendo vyovyote vinavyoweza kupelekea uhalifu kwenye wilaya yetu.” Amesema Ibrahimu.

Sauti ya SSP Ibrahim Idd Abdala.

Awali wananchi wa kijiji cha Bahi Sokoni walipata nafasi ya kuelezea changamoto zinazowakabili na kumuomba mkuu wa wilaya awasaidie kuzitatua huku mkazi wa kitongoji cha kichangani Rosemary Makala akiomba kulipwa eneo aliloachiwa na marehemu mumewe ili aweze kusomesha watoto wake.

Sauti ya Rosemary Makala.