Dodoma FM

TASAC labainisha kutekeleza miongozo inayotolewa na serikali

8 March 2023, 11:19 am

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Bw. Kaimu Mkeyenge leo Machi 7, 2023 Jijini Dodoma.Picha na Maelezo

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limebainisha kuwa linatekeleza miongozo inayotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Na Mindi Joseph.

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limebainisha kuwa inatekeleza miongozo inayotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) katika kuhakikisha manunuzi, matumizi bora, sahihi na salama ya vifaa na mifumo yote ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Serikalini yanazingatiwa.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Bw. Kaimu Mkeyenge leo Machi 7, 2023 Jijini Dodoma, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya TASAC, pamoja na kubainisha Mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka miwili ya mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Sauti ya mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Bw. Kaimu Mkeyenge.

Mkeyenge amesema kuwa TASAC imeunganisha ofisi zake zote zikiwemo zile za Mikoa, Wilaya na mipakani kwenye Mkongo wa Taifa ambao umerahisisha na kuharakisha mawasiliano ya ndani (Intranet), barua pepe, na mawasiliano na wadau wa nje .

Sauti ya mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Bw. Kaimu Mkeyenge.

Aidha , Mkeyenge ameongeza kuwa uendelezaji wa miundombinu na mifumo ya TEHAMA ulianza mwaka wa fedha 2018/19 na utakamilika mwaka wa fedha 2025/26 huku mifumo ambayo inayoboreshwa ndani ya Shirika ni pamoja na mfumo wa ukaguzi, usajili wa vyombo vya usafiri kwa njia ya maji na utoaji wa vyeti vya Mabaharia (Maritime Administration Management System), mfumo wa utoaji leseni, ukusanyaji wa mapato ya udhibiti, uhakiki kadhia na kutoa ankara za malipo ya watoa huduma wa meli (Manifest Billing System), pamoja na mfumo wa kutoa huduma za biashara ya Meli.