Dodoma FM

Bahi wajipanga kutinga tano bora matokeo darasa la saba kitaifa

27 February 2023, 3:33 pm

Mheshimiwa Godwin Gondwe mkuu wa wilaya ya Bahi.Picha na Benard Magawa

Mheshimiwa Godwin Gondwe akiongoza wadau wa elimu wilayani Bahi katika hafla ya kufanya tathmini ya elimu na kutoa tuzo kwa shule, walimu na wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma.

Na Benard Magawa

Mkuu wa wilaya ya Bahi Mheshimiwa Godwin Gondwe amewaongoza wadau wa elimu wilayani Bahi katika hafla ya kufanya tathmini ya elimu na kutoa tuzo kwa shule, walimu na wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma kufuatia wilaya hiyo kushika nafasi ya kumi kitaifa katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2022.

Mheshimiwa Godwin Gondwe akitoa tuzo kwa shule, walimu na wanafunzi.Picha na Benard Magawa

Hafla hiyo iliyohudhuriwa na waheshimiwa Madiwani, wakuu wa Taasisi mbalimbali, viongozi wa dini,watendaji wa kata na wadau mbalimbali wa elimu imefanyika Februari 24,2023 katika viwanja vya Halmashauri ya wilaya ya Bahi huku ikiweka mikakati ya kushika nafasi ya tano kitaifa kwa mwaka 2023.

Pongezi hizo zilijumuisha walimu wa shule za Sekondari wilayani Bahi, ambazo katika matokeo ya kidato cha pili ya Novemba 2022 idara hiyo iliibuka na ushindi wa nafasi ya pili kati ya wilaya nane za Mkoa wa Dodoma.

Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mheshimiwa Godwin Gondwe ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amewahimiza wadau wa elimu wilayani humo kushirikiana na kudhamiria kutorudi nyuma ili kupanda na ikiwezekana kushika nafasi ya juu zaidi.

Lazima tuangalie mapungufu tuliyobakiza na tuyafanyie kazi, ili tujazilize ikiwezekana tushike nafasi ya kwanza kitaifa

“Lazima tuangalie mapungufu tuliyobakiza na tuyafanyie kazi, ili tujazilize ikiwezekana tushike nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo yajayo na inawezekana tukishikamana na kufanya kazi kwa pamoja.” Amesema Gondwe.

Sauti ya Mheshimiwa Godwin Gondwe.

Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM taifa (MNEC), ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bahi Mheshimiwa Donald Mejiti amesema wataweka utaratibu wa kutoa tuzo kila mwaka kwa wanafunzi na walimu ili kujenga ari na mwamko wa elimu wilayani humo.

“Tuzo kama hizi nashauri viongozi tuzitoe kila mwaka naamini tutaweka historia, pia tutaongeza uwajibikaji kwa walimu na wanafunzi wakiamini kila atakayefanya vizuri atatuzwa, pia wazazi watapata uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa elimu, kwakufanya hivyo tutapiga hatua kubwa kielimu.” Amesema Mejiti.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bahi Mheshimiwa Donald Mejiti.

Naye Afisa elimu Msingi wa wilaya hiyo Boniface Wilson amesema kwa mwaka 2023 halmashauri imejipanga kuhakikisha inashika nafasi ya tano kitaifa huku akiweka bayana mikakati iliyoandaliwa na idara hiyo kuhakikisha wanaingia tano bora kwa mwaka 2023 katika matokeo ya darasa la saba.

Afisa elimu Msingi Boniface Wilson.