Dodoma FM

Marufuku walimu wa kiume kutumika kusindikiza magari ya shule (School bus)

20 February 2023, 6:00 pm

kikao kilichoratibiwa na Ofisi ya katibu tawala mkoa wa Dodoma.Picha na Alfred Bulahya

KATIKA kukabilina na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto nchini mkoa wa Dodoma umepiga marufuku walimu wa kiume kutumika kusindikiza magari ya shule (School bus) na kuanzia sasa wanawake pekee ndiyo watakao husika na jukumu hilo.

Na Alfred Bulahya.

Marufuku hiyo ilitolewa juzi kwenye kikao kilichoratibiwa na Afisa ustawi wa Jamii mkoa wa Dodoma, kilichojumuisha walezi wa vituo vya kulelea watoto (Day care),walezi wa makao ya watoto pamoja na wamiliki wa shule na vituo hivyo kutoka halmashauri zote za mkoa huo.

Afisa ustawi wa Jamii mkoa wa Dodoma Josephine Mwaipopo.

Afisa ustawi wa Jamii mkoa wa Dodoma, Josephine Mwaipopo,akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho alisema lengo kuu ni kuwajengea uwezo walezi pamoja na wamiliki wa makao ya watoto pamoja na vituo vya kulelea watoto kuhusu sheria,miongozo na kanuni za nchi.

Alisema pamoja na kuwajengea uwezo kikao hicho kimehitimishwa kwa kuwekwa maazimio mbalimbali ikiwemo walimu wa kike kutumika kusindikiza magari ya shule badala ya wanaume.

Kikao hichi kimehusisha walezi na wamiliki zaidi ya 200 ambapo mwisho tumekuja na maadhimio ikiwemo walimu wa kiume tangu sasa hawata ruhusiwa kusindikiza gari za shule watakao tumika ni walimu wa kike na tunapanga kuona ni jinsi gani hata madereva ambao watatumika kuendesha hizi ‘School bus’ wawe wanawake pia.

“Siyo kama hatuwaamini walimu wa kiume tena lakini kutokana na tabia za wanaume wachache zimeharibu sifa za wanaume wengine hivyo kwanzia sasa mkoani kwetu walimu wa kike ndiyo tutawatumia ili kupunguza matukio haya ya ukatili kwa watoto hasa katika vitendo vya ulawiti pamoja na unajisi”

alisema Mwaipopo.

Aidha, alisema azimio jingine ni kwa vito vyote vya kulelea watoto pamoja na makao ya watoto ambvyo havijasajiliwa vifanye hivyo ndani ya miezi mitatu na baada ya hapo hatua za kisheria zitachukuliwa.

Alisema zaidi ya asilimia 60 ya vituo vya kulelea watoto pamoja na makao ya watoto havijasajiliwa hivyo kuendeshwa kinyume cha sheria,kanuni na miongozo ya nchi.

“Tumekubaliana kwa pamoja hivi vituo vyote pamoja na makao ya watoto ambavyo bado havina usajili wa serikali kukamilisha usajili ndani ya miezi mitatu na baada ya hapo atakayeshindwa kutimiza maelekezo hayo tutamfungia kutoa huduma”

alisema Mwaipopo.

Kadhalika, alisema wamekubaliana kila robo ya mwaka watakuwa wanakutana kujadiliana fursa na vikwazo pamoja na kutathimini maadhimio waliyojiwekea.

“Lakini katika kikao hichi pia tumewafundisha walezi kuacha kutumia nguvu kuwafundisha watoto wadogo kwakua umri wa kuanzia mwaka sifuri hadi miaka nane wanajifundisha kwa njia za fahamu hivyo ni bora wakawacha wajifunze kwa kusikia,kuona pamoja na kucheza ili wasiharibu ubongo wa watoto”

alisisitiza Mwaipopo.

Hata hivyo, alizitaka shule pamoja na vituo hivyo kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya saa 24 kila yanapotokea na atakaye shindwa kufanya hivyo atachukuliwa kama sehemu ya ukatili huo.

“Toeni taarifa kila matukio ya ukatili yanapotokea kwenye maeneo yenu,kuna mtu anaweza kusema anaogopa kuharibu taswira ya shule yake lakini tukibaini kuwa umeficha taarifa tutakuchukulia hatua kwa mwijibu wa sheria”alisema