Dodoma FM

Wakulima walalamikia wafanyabiashara wa mchele Bahi

10 February 2023, 4:52 pm

Wakulima wa mpunga wilayani Bahi mkoani Dodoma wamelalamikia wafanya biashara wanaofuata mchele na Mpunga.Picha na Pixel

Wakulima wa mpunga wilayani Bahi mkoani Dodoma wamelalamikia wafanya biashara wanaofuata mchele na Mpunga unaozalishwa wilayani humo kwa kuupa majina ya mchele wa mikoa mingine wanapouuza katika masoko mbalimbali hapa nchini tatizo linalopelekea kutotambulika kabisa kwa mchele wa Bahi kwenye masoko hapa nchini.

Na Benard Magawa.

Wakulima hao wameyasema hayo mapema hii leo Februari 10, 2023 wilayani humo wakiiomba serikali na mashirika mbalimbali kuona namna ya kuwasaidia ili mpunga unaolimwa katika bonde la Bahi kutambulishwa katika masoko kwani mchele unaotoka hapo una kiwango cha juu na unalimwa bila kutumia mbolea.

Wakizungumza kwa masikitiko kuhusiana na suala hilo wamesema kumekuwa na tabia ya wafanyabiashara wanaotoka maeneo mbalimbali hapa nchini kufuata bidhaa hiyo wilayani hapo kutoweka nembo za jina la mchele wa Bahi na kuupa jina la mchele unaotoka mikoa mingine wakati mchele huo umetoka Bahi.

“ Wafanyabiashara wanaofuata mchele kwetu wamekuwa na tabia ya kuweka lebo ya mchele unaotoka mikoa mingine pindi wanapouza katika masoko badala ya kuweka nembo ya supa Bahi’’

“Tunaomba serikali itusaidie ili nasi mchele wetu uweze kutambulika katika masoko mbali mbali hapa nchini kwani tunazalisha mchele wenye kiwango cha juu sana.”

Walisema.

Wameeleza kuwa Bahi kuna mchele mzuri kama vile supa Zambia, Nganyalo pamoja na Mbawa mbili lakini hakuna soko lolote hapa nchini unaweza kukuta nembo za mchele huo kitu ambacho ni kudhurumu haki za wakulima wa Bahi.

“ Mchele unaotoka Bahi ni mzuri sana na unalisha karibia mkoa mzima wa Dodoma na maeneo mengine hapa nchini lakini tunashangaa wafanyabiashara wa masoko yote hapa nchini unakuta wameuwekea nembo za mchele unaotoka mikoa mingine kama vile mbeya na shinyanga wakati ukiutazama unaona kabisa ni nganyalo na supa Zambia ya Bahi,”

Walisema.

Wilaya ya Bahi ni miongoni mwa wilaya zinazozalisha mpunga kwa wingi hapa nchini ambapo inakadiriwa kuwa na zaidi ya ekari laki tatu ambazo hutoa zaidi ya tani laki tisa kwa mwaka huku ikielezwa kuwa pamoja na kiwango kikubwa cha mpunga unaozalishwa wilayani Bahi lakini mchele wa Bahi haupatikani kwenye soko lolote hapa nchini japo kiuhalisia mchele huo upo kwenye masoko mengi.