Dodoma FM

Wizara ya Ardhi kutoa hatimiliki

23 January 2023, 10:25 am

Na; Seleman Kodima.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) inatarajia kutoa Hati Milki za Ardhi milioni moja katika maeneo ya mijini pamoja na Hati Miliki za Kimila laki tano kwenye maeneo ya vijijini.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa mradi wa LTIP Joseph Shewiyo wakati wa semina ya siku moja na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi iliyofanyika jijini Dodoma.

Amesema, kazi ya utoaji hati miliki kwenye maeneo ya mijini itafanyika kwa kutumia watumishi wa serikali kwa asilimia 20 huku asilimia 80 iliyobaki ikifanywa na makampuni yaliyosajiliwa kufanya kazi ya kupanga na kupima.

Akielezea upande wa Hati Milki za Kimila, Mratibu huyo wa LTIP amesema, kazi hiyo itafanywa na watumishi wa serikali na taasisi zisizo za kiserikali na kubainisha kuwa kazi itakayofanyika ni pamoja na kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji 250 na utoaji hati milki laki tano za kimila.

Aidha amewaeleza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii iliyojumisha pia Wabunge wanaotoka halmashauri ambazo mradi huo utaanza kwa mwaka wa kwanza kuwa, mradi wa LTIP utekelezaji wake utakuwa na shughuli mbalimbali na kuzitaja kuwa ni pamoja na utoaji Hati, maandalizi ya ramani za msingi, uboreshaji mfumo wa ILMIS, Alama za msingi na mifumo ya uthamini sambamba na ujenzi wa ofisi za ardhi za mikoa 25.

Kwa upande wao, Wabunge wametaka utekelezaji Mradi huo wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi nchini uende sambamba na utoaji elimu kwa wananchi hasa wanawake pamoja na watendaji wa serikali kuanzia ngazi ya mitaa ili kuleta ufanisi zaidi katika mradi.