Dodoma FM

Taasisi za lishe zatakiwa kubadilishana uzoefu ili kupambana na utapiamlo

11 May 2022, 2:34 pm

Na; Selemani Kodima.

Wizara na Taasisi zinazohusiana na masuala ya lishe nchini zimetakiwa kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika mapambano dhidi ya Utapiamlo kuhakikisha jamii na Taifa linakuwa salama.

Akizungumza katika mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu Mpango wa Pili  Jumuishi wa Masuala ya Lishe wa Kitaifa kwa Menejimenti ya Sekta ya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Ukumbi wa Wizara hiyo  Jijini Dodoma

.

Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Lishe kutoka Shirika la Marekani la Maendeleo Kimataifa (USAID) Bi. Debora Niyeha amesema mpango huo unaanza utekelezaji wake mwaka 2021-2022/ 2025-2026 hivyo kama sekta ya mifugo ina sehemu ya kufanya kuhakikisha malengo ya mpango huo yanafikiwa.

.

Aidha ameitaja mikoa inayoongoza kwa utapiamlo licha ya kuwa na kiwango  kikubwa cha uzalishaji wa chakula alitaja kuwa ni mikoa  saba ikiwemo ya Njombe, Ruvuma, Mbeya na Iringa ambapo zaidi ya asilimia 40 ya watoto wana udumavu unaoathiri hata uwezo wao kimasomo.

.

Kwa upande wake  Mkurugenzi  Msaidizi Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bi. Devotha Gabriel amebainisha kwamba kuendelea kupungua kwa udumavu kumetokana na utekelezwaji wa mpango wa kwanza huku akisema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo waratibu hivyo iko tayari kushiriki kikamilifu katika jitihada hizo.

.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Sekta ya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Mhina aliishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kutoa elimu hiyo muhimu itakayowajengea uwezo sekta hiyo.