Dodoma FM

Wazazi watakiwa kuwapeleka watoto katika vituo vya Afya

6 April 2022, 3:22 pm

Na;Yussuph Hassan.

Wazazi na walezi Mkoani Dodoma wameshauriwa kuhakikisha wanawapeleka Watoto wao katika vituo vya afya kufanya uchunguzi wa Magonjwa mbalimbali ambayo mara nyingi huwa kama yamesahauliwa katika jamii.

Akizungumza na kituo hiki Dkt Matthew Gaudance kutoka kituo cha Afya cha Decca Pollyclinic Dodoma amesema kuna magonjwa mbalimbali ambayo hayapewi kipaumbele katika jamii hivyo ni vyema jamii ikajenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa kina.

Ameongeza kuwa  Magonjwa ya kurithi kama Seli mundu yanapaswa kudhibitiwa mapema kabla athari yake haijawa kubwa.

Taswira ya habari imezungumza na baadhi ya akina Mama Jijini Dodoma ambapo baadhi yao wamedai kuwa kuwepo kwa gharama kubwa za matibabu katika baadhi ya vituo vya afya ni chanzo cha kukwepa kuwapeleka watoto wao hospitali.

Watoto wamekuwa wanakumbwa na magonjwa mbalimbali katika kipindi chao cha ukuwaji kutokana na mfumo wao wa kinga kuwa chini hivyo ni vyema wazazi au walezi kutodharau dalili za hali wanazopata watoto hao.