Dodoma FM

Wakazi wa mtaa wa Itega walalamikia kuzagaa kwa takataka

1 April 2022, 2:31 pm

Na; Neema Shirima.

Wananchi wa mtaa wa Itega kata ya Nkuhungu jijini Dodoma wamelalamikia suala la kuzagaa kwa takataka katika maeneo hayo kutokana na kutokuwepo gari ya kuzoa takataka hizo.

Wakizungumza na taswira ya habari wananchi hao wamesema magari yanayojishughulisha na ukusanyaji wa takataka yamekuwa hayafiki kwa wakati na wakati mwingine kutofika kabisa hali inayosababisha taka hizo kuzagaa hovyo ambapo wameiomba serikali iwasaidie waweze kuondokana na changamoto hiyo ambayo ni hatari kwa afya zao.

Aidha mwenyekiti wa mtaa huo bwn Casian Mponela amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo ambapo amesema awali alikuwepo  mzabuni ambaye alikuwa na mkataba wa kufanya kazi hiyo ya kuzoa taka lakini kwa sasa amevunja mkataba huo hivyo kupelekea uwepo wa changamoto hiyo.

Ameongeza kuwa kwa sasa tayari wameshapewa barua kwaajili ya kutafuta mzabuni mwingine hivyo amewasihi wananchi wa mtaa huo pamoja na kata nzima ya Nkuhungu kuwa wavumilivu kwani changamoto hiyo itatatuliwa hivi karibuni.

Tunza mazingira yakutunze, ni usemi ambayo wengi hupenda kuutumia hivyo ni vema kila mwananchi kuhakikisha ana safisha mazingira  yanayomzunguka ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko.