Dodoma FM

Hali ya ugonjwa wa kifua kikuu yaendelea kudhibitiwa

23 March 2022, 2:39 pm

Na;Yussuph Hassan.  

Kuelekea siku ya kifua kikuu Duniani march 24, imeelezwa kwa Serikali Mkoani  Dodoma katika kutokomeza ugonjwa huo ilipanga kila baada ya miezi mitatu kuibua wagonjwa Elfu Moja, Mitatu Sitini na Mbili, kila baada ya miezi mitatu.

Lengo hilo ambalo mpaka kufikia sasa limefikiwa kwa asilimia 75 huku wakiendelea na mpango wa kuongeza kasi kwa wiki moja iliyosalia kumalizika kwa mwezi wa tatu.

Akizungumza na kituo hiki Mratibu wa kifua kikuu Mkoani Dodoma Dkt Peres Lukango amesema hali ya ugonjwa wa kifua kikuu inaendelea kudhibitiwa na kuhakikisha jamii inakuwa na elimu ya kina juu ya ugonjwa huo.

Ameongeza kuwa katika kutafuta wagonjwa wapya, serikali imeendelea kuimarisha mfumo wa takwimu kuhakikisha wagonjwa wa zamani wanaingizwa kwenye mfumo ili kujua ukubwa wa tatizo.

Aidha Dkt Lukango ameelezea namna ugonjwa huo unavyoambukizwa ambapo ni kwa njia ya hewa kutoka kwa mtu mmoja aliyeambukizwa kwenda kwa mtu mwengine.

Kifua Kikuu (TB) ni miongoni mwa magonjwa hatari zaidi duniani , ambapo kila ifikapo March 24 ya kila mwaka Dunia inaadhimisha siku ya kifua kikuu, kitaifa yananyika Mkoani Tanga yakienda sambamba na kauli mbiu isemayo Okoa maisha, wekeza katika kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu Nchini.