Dodoma FM

Mgogoro kati ya Urusi na Ukraine watajwa kuleta athari za kiuchumi

3 March 2022, 2:11 pm

Na; Benard Filbert.

Mgogoro unaoendelea hivi sasa kati ya Urusi na Ukraine umetajwa kuleta athari kubwa za kiuchumi barani Afrika ikiwepo kupanda kwa bei ya nishati ya mafuta.

Hayo yameelezwa na Profesa Enock Wiketie mchambuzi wa masuala ya uchumi kutoka chuo kikuu cha Iringa wakati akizungumza na taswira ya habari.

Profesa Wiketie amesema Urusi ni miongoni mwa nchi ambayo inazalisha mafuta ya Petrol na Gesi kwa wingi ambayo inauzwa katik nchi nyingi Duniani hivyo kutokana na vikwazo inavyowekewa hivi sasa itakuwa ngumu kufanyika kwa biashara hiyo.

Kadhalika amesema uhusiano wa kidiplomasia kati ya Urusi na nchi zingine utapungua kwa kiasi kikubwa kwani nchi hiyo inategemea kufanya biashara na nchi nyingine.

Katika jitihada za kupambana na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi yake na Mataifa mbalimbali, Serikali ya Urusi imetangaza kiwango kipya cha pesa ambacho Mtu anaweza kutuma nje ya Urusi Kwa Wakazi/raia wa Urusi kuanzia sasa hawatoruhusiwa kutuma nje ya Nchi zaidi ya $ 10000 (Tsh. milioni 23) na wasio Wakazi/Raia hawatoruhusiwa kutuma nje ya Nchi $5000 (Tsh. milioni 11.5)