Dodoma FM

Ucheleweshaji wa miradi hurudisha nyuma matumaini ya wananchi

27 January 2022, 3:34 pm

Na; Thadei Tesha.

Imeelezwa kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea mwitikio wa wananchi kuchangia nguvu kazi katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo kuwa mdogo  ni pamoja na baadhi ya viongozi kusuasua kukamilisha miradi hiyo.

Taswira ya habari imefanya mahojiano na baadhi ya wananchi jijini hapa kufahamu ni kwa kiasi gani wamekuwa wakijitolea nguvu kazi katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo.

Wamesema kwa sasa mwitikio umekuwa si wa kuridhisha kwani baadhi ya viongozi wamekuwa wazito kukamilisha miradi inayoanzishwa na wananchi ikiwa ni pamoja na majukumu kwa wananchi kuwa mengi.

Baadhi ya viongozi wa mitaa akiwemo mwenyekiti wa mtaa wa kiwanja cha ndege jijini hapa amesema ingawa suala la kuchangia maendeleo ikiwemo kujenga shule pamoja na miundombinu imekuwa ikitekelezwa na serikali lakini pia wananchi wanaweza kushiriki suala hilo kwa lengo la kuleta maendeleo katika jamii.

Aidha ametoa wito kwa viongozi wa serikali kuendeleza juhudi za wananchi ambazo zimekuwa zikitekelezwa katika mitaa mbalimbali ili kuendelea kuleta hamasa zaidi kwa wananchi juu ya suala hilo.

Nguvu kazi imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambapo wananchi wamekuwa wakihamasisha viongozi kuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi hizo.