Dodoma FM

Wakazi wa Ihumwa waomba elimu ya urasimishaji Ardhi iongezwe kwa wananchi

20 January 2022, 4:18 pm

Na; Neema Shirima.

Imeelezwa kuwa licha ya kutolewa elimu katika baadhi ya maeneo ya Dodoma kuhusiana na suala la upimaji na urasimishaji wa maeneo bado baadhi ya wananchi hawajapata elimu ya kutosha kuhusiana na zoezi hilo.

Hayo yamebainishwa na bwn Petro Mpolo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya upimaji katika mtaa wa Chang’ombe kata ya Ihumwa jijini Dodoma ambapo amesema mbali na kutolewa elimu bado kuna baadhi ya wananchi wa mtaa huo wamekuwa waking’oa alama za upimaji maarufu kama bikoni

Aidha kwa upande wake  bi Evelina Mbalai ambaye ni mwananchi amesema wanatambua kuwa ni kosa kisheria kung’oa bikoni na ameiomba serikali iendelee kutoa elimu zaidi kuhusiana na zoezi hilo ili ambao bado hawajapata uelewa huo waweze kuupata.

Naye bwn Gilbert Mkenangwa ambaye ni meneja msaidizi wa kampuni ya upimaji ameshauri wananchi wa mtaa huo kuwa wavumilivu katika kipindi cha zoezi la urasimishaji kwani kwa kufanya hivyo kutawapa manufaa katika ardhi wanazozimiliki na hatimae kujenga kwa uhakika ili kuepuka changamoto za ubomolewaji wa nyumba zao

Mtaa wa chang’ombe upo katika kata ya Ihumwa jijini Dodoma ambapo kwa sasa upo katika zoezi la urasimishaji wa maeneo na changamoto kubwa ni ukosefu wa elimu ya kutosha juu ya zoezi hilo kwani baadhi ya wakazi wa mtaa huo wamekua wakijenga bila kufata taratibu za ujenzi