Dodoma FM

Taasisi zatakiwa kuwapatia vijana mbinu za kujikwamua kiuchumi.

20 January 2022, 4:36 pm

Na; Thadei Tesha.

Taasisi mbalimbali za binafsi na serikali zimetakiwa kushirikiana na viongozi wa dini ili kuwasadia vijana katika kuwapa mbinu mbalimbali za maisha ili kujikwamua kiuchumi.

Taswira ya habari imefanya mahojiano na baadhi ya viongozi wa dini kutoka sehemu mbalimbali jijini hapa kufahamu ni kwa kiasi gani wamekuwa wakishirikiana na jamii katika kuwasaidia vijana kuwapa fursa mbalimbali za kujikwamua kiuchumi.

Ibrahimu Mwamed ni moja ya viongozi wa dini ambaye ni mchungaji kutoka katika kanisa la EAGT Ndachi amesema wao kama kanisa wameanzisha programu ya kuwasaidia vijana kuhusiana na masuala mbalimbali ambapo pia ametoa wito kwa madhehebu mengine kuiga mfano huo.

Kwa upande wake mchungaji Antony Wambura kutoka kanisa la Tanzania Assembies Of God Bahi amesema viongozi wa dini wanayo nafasi kubwa kuelimisha jamii kuhusiana na masuala mbalimbali ili kupunguza vitendo vya kikatili katika jamii pamoja na kuwajengea vijana kuwa na hofu ya Mungu.

Kwa upande wao baadhi ya vijana jijini hapa wamesema viongozi wa dini wanayo nafasi kubwa ya kuwasaidia kwani wapo baadhi ya vijana ambao tayari wameshanufaika kupitia miradi mbalimbali inayoanzishwa na kanisa.

Mara kadhaa vijana wamekuwa wakinufaika kutokana na taasisi mbalimbali za kidini kuwapa kipaumbele katika fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushirikiana na serikali jambo ambalo limewasaidia kujikwamua kiuchumi.